NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

Katika kuimarisha usalama wa wanafunzi barabarani, kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania Limited kwa kushirikiana na TotalEnergies Foundation na NafasiArt Space, wamezindua rasmi mradi wa VIA Creative kwa mwaka 2025 ambao unatumia sanaa ya muziki, maigizo na njia bunifu kuelimisha na kuwahamasisha wanafunzi kuhusu usalama barabarani.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi huo leo Julai 25, 2025 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Temeke, Saadati Mohamed ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, amewapongeza TotalEnergies kwa kuendeleza dhamira ya dhati ya kulinda usalama wa vijana na kuwawezesha kielimu.

Amesema usalama barabarani si suala la barabara nzuri pekee, bali pia linahitaji uelewa wa sheria, tabia sahihi na ushirikiano wa jamii nzima.

“Kila mwaka maisha ya watu, wakiwemo wanafunzi, hupotea kutokana na ajali zinazoweza kuzuilika. Mradi huu wa VIA Creative ni wa kipekee na wa kupongezwa kwa kutumia sanaa kuelimisha kuhusu usalama barabarani,” amesema Mohamed.

Aidha, amesema amefurahishwa na hatua hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa vijana wa sekondari ni miongoni mwa watumiaji wakuu wa barabara, wengi wao wakitembea kwa miguu, kuendesha baiskeli au kutumia bodaboda ambazo zimekuwa chanzo kikuu cha ajali nyingi.

“Ni faraja kuona kuwa jitihada hizi zinaenda sambamba na juhudi za serikali, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, na wadau wengine katika kuhakikisha ajali barabarani zinapungua,” ameongeza Mohamed.

Amesema kuwa kwa kuwapa wanafunzi elimu ya usalama barabarani mapema, taifa linaweka msingi wa kizazi kinachojali usalama na hivyo kuchangia maendeleo endelevu.

Pamoja na hayo amehimiza taasisi nyingine binafsi kuiga mfano wa TotalEnergies kwa kuwekeza katika elimu ya usalama na maendeleo ya kijamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa sheria na uhusiano TotalEnergies Getrude Mpangile amesema kuwa kuanzia mwaka 2022 hadi 2024, VIA Creative ililenga wanafunzi wa shule za msingi na kufikia zaidi ya wanafunzi 22,000 katika shule 60 zilizopo Dar es Salaam, Mkoa wa Pwani, na Morogoro. Na leo hii wamepanua zaidi lengo la mradi huu kwa kufikia wanafunzi wa sekondari wakianza na
shule ya Sekondari Ndalala na kuongeza mkoa wa Dodoma.

Amesema kupitia mradi huo, wanafunzi watapata fursa ya kushiriki katika shindano la kitaifa, wakionyesha maarifa ya usalama barabarani na ujuzi walioupata.

"Shule itakayoshinda kitaifa itapata heshima ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kikanda, jambo linaloleta fahari ya kitaifa na pia ushirikiano wa kikanda juu ya maadili ya usalama barabarani" amesema Getrude

Amesema kuwa washindi wa kitaifa wa shindano la VIA Creative watapatiwa utekelezaji wa pendekezo au mapendekezo watakayo toa kwaajili ya uboreshaji wa usalama wa barabarani.

"Hatua ilitekelezwa kwa mara ya kwanzia kwenye tolea la mradi huu mwaka 2024 ambapo shule ya msingi ya Makuburi walipendekeza kujengewa Ukuta wa shule ambao tulishanikiwa kufanikisha na leo hii shule ya msingi ya Makuburi ina Uzuio unaowalinda wanafunzi dhidi ya magari na boda boda zilizokuwa zikipita na kuegeshwa kwenye uwanja shule" ameeleza.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...