Na Jackson Isdory, CMU

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeendeleza rekodi yake ya ubora katika nyanja za elimu, utafiti na ubunifu baada ya kutangazwa Mshindi wa Kwanza katika kundi la Taasisi za Elimu ya Juu, Uendelezaji Ujuzi na Utafiti kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama Sabasaba, yaliyofanyika kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2025.


Tuzo hiyo yenye heshima kubwa ilikabidhiwa rasmi na Mhe. Dkt. Selemani Saidi Jafo. Waziri wa Viwanda na Biashara, ikishuhudiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, ambaye pia ni mhitimu wakuheshimika wa UDSM, katika hafla ya kufunga maonesho hayo iliyofanyika kwenye Viwanja vya Sabasaba Dar es Salaam.


Tuzo hii ni uthibitisho wa dhamira thabiti ya UDSM katika kuchochea maendeleo ya uchumi wa maarifa nchini kupitia utafiti wa kisasa, uwezeshaji wa ujuzi na ubunifu unaojibu mahitaji ya jamii. Katika hotuba yake ya kufunga maonesho, Waziri Mkuu Majaliwa aliipongeza Sabasaba kwa kuwa jukwaa muhimu la kitaifa la ubunifu, uwekezaji na ushirikiano, akisema “Maonesho haya si tukio tu, bali ni jukwaa la kimkakati. Tunapaswa kujifunza kutoka kwa wenzetu duniani, kama vile Japan Expo ambako Tanzania iliwakilishwa vyema.”



Aliwahimiza Watanzania kuunga mkono bidhaa na maudhui ya ndani kwa lengo la kujenga uchumi wa kujitegemea na wenye ushindani. “Lazima tukumbatie bidhaa, ubunifu na chapa za Kitanzania kama ambavyo TanTrade inaendeleza ajenda ya ‘Made in Tanzania’. Taasisi zilizoshinda zina nafasi muhimu katika kufanikisha jambo hili,” alihimiza Waziri Mkuu.


●Hatua Muhimu ya Mafanikio


Akizungumza kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Anangisye, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Utafiti, Prof. Nelson Boniface, alisema tuzo hiyo ni mafanikio makubwa na pia mwito mpya wa kutimiza wajibu. “Tuzo hii ni ya kila mwanafunzi, msomi, mtafiti, mwasilishaji na mshirika wetu. Ni alama ya kile tunachoweza kufanikisha tukifanya kazi kwa pamoja kwa maono ya pamoja.”



Katika kipindi chote cha maonesho, banda la UDSM liliwavutia maelfu ya wageni wa ndani na kimataifa kupitia nishati yake ya ubunifu, miradi yenye uhalisia na maonesho ya vitendo. Chuo kilionyesha matokeo ya tafiti na teknolojia bunifu katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, afya, elimu, uhandisi, nishati mbadala, usafi wa maji, na jiolojia na madini.


“Ubunifu mwingi uliowasilishwa umetengenezwa na wanafunzi na watafiti vijana, jambo linaloonesha dhamira ya UDSM kukuza vipaji vya vijana,” alisisitiza Prof. Boniface.




Moja ya mafanikio yaliyowasisimua watu wengi ni kifaa kilichobuniwa na mwanafunzi wa kike Bi. Nurath Nurdin, kifaa hicho huchunguza damu bila kutumia sindano, kwa kutumia sensa ya mwanga na akili bandia kupima vipimo vya damu kupitia kwenye ngozi. Teknolojia hii ni suluhisho mbadala salama kwa watu wenye maradhi ya muda mrefu kama kisukari.


●Ubunifu wa Kisasa na Miradi Yenye Tija



Mbali na viongozi wa serikali na wasomi, banda la UDSM lilipata heshima ya kutembelewa na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kansela wa sasa wa UDSM. Alizungumza na wabunifu vijana, akionesha kuvutiwa na ubunifu na umuhimu wa miradi iliyowasilishwa. Ziara yake iliwatia moyo wanafunzi na watumishi, ikiendeleza urithi wa UDSM wa kulea viongozi wa kitaifa na watatuzi wa changamoto.



Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya UDSM Sabasaba, Dkt. Dotto Paul Kuhenga, ambaye pia ni Mkuu wa Mawasiliano na Masoko wa UDSM, alieleza kuridhishwa sana na mafanikio ya chuo kwenye maonesho haya.


“Ushindi huu umetokana na mshikamano, mipango madhubuti na dhamira ya kweli. Ni ushahidi wa utamaduni wa ubora na dira ya UDSM ya kuangalia mbele. Nawapongeza wote walioshiriki, vitivo, idara na ofisi zote, kwa kuwasilisha maonesho ya kiwango cha kimataifa,” alisema.


Mitandao ya kijamii ilifurika pongezi, wengi wakieleza kuwa banda la UDSM lilikuwa moja ya mabanda yenye mvuto, ubunifu na uhalisia mkubwa katika maonesho hayo. “Ni mfano hai wa namna tafiti, ubunifu na uwezeshaji wa vijana vinavyoweza kushirikishwa kwa ajili ya maendeleo ya taifa,” aliandika mgeni mmoja.


Zaidi ya maonesho ya vitu, UDSM pia liliendesha vipindi vya mafunzo kila siku, ikiwemo mawasilisho ya programu za shahada na uzamili, ushauri wa biashara, huduma za afya, ushindani wa ubunifu wa wanafunzi na majadiliano na wanachuo waliomaliza masomo. Hii iliunda jukwaa la ushirikiano baina ya elimu ya juu, sekta binafsi, serikali na jamii kwa ujumla.


Kwa hakika ushindi na tuzo hii inathibitisha tena nafasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama kinara barani Afrika katika elimu ya juu, utafiti na ubunifu. UDSM itaendelea kulea vipaji, kuchochea maendeleo jumuishi na endelevu, na kugeuza maarifa kuwa matokeo halisi kwa Tanzania na dunia kwa ujumla.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...