Na Seif Mangwangi, Arusha

KUELEKEA Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na Rais Oktoba mwaka huu 2025, Baraza la Habari Tanzania (MCT), limetoa mwongozo kwa Waandishi wa habari wanaojihusisha na siasa kwa kugombea nafasi mbalimbali uongozi na kuwataka kuacha kazi hiyo ili kuleta usawa.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Julai2, 2025 Jijini hapa, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Ernest Sungura amesema waandishi wa habari kugombea nafasi za kisiasa huku wakiendelea kufanyakazi za kiuandishi ni ukiukwaji wa maadili ya taaluma ya habari na kuvunja uaminifu kwa jamii.

" Waandishi wa habari wanaogombea huku wakiendelea na kazi yao wanakabiliwa na athari kubwa kwa taaluma yao na tasnia ya habari kwa ujumla. Kwanza, kuna suala la kupoteza uaminifu. Wananchi na vyombo vingine vya habari hawawezi kumwamini mwandishi ambaye anaegemea upande wa kisiasa, kwani taarifa zake zitaonekana kuwa na upendeleo au ajenda ya kisiasa badala ya ukweli na uwazi," amesema Sungura.

Amesema pili, mwandishi anayegombea atakuwa na mgongano wa maslahi. "Mwandishi hawezi kuripoti kwa haki na usawa akiwa ana maslahi binafsi katika uchaguzi, kwani anaweza kushawishika kuandika kwa faida yake au chama chake badala ya kuzingatia ukweli na maadili ya uandishi wa habari" amesema.

Sungura amesema pia kuchanganya siasa na uandishi wa habari kunaharibu tasnia ya habari kwa kuifanya kuwa chombo cha propaganda badala ya kuwa chanzo cha taarifa sahihi na kusema hali hiyo inapunguza hadhi ya taaluma ya uandishi wa habari na kuathiri uwezo wa vyombo vya habari kutoa taarifa kwa uwazi na bila upendeleo.

"Kwa kuzingatia athari hizi, mwandishi wa habari anayegombea nafasi ya kisiasa anapaswa kujiondoa rasmi kwenye chumba cha habari ili kuepuka mgongano huo wa kimaslahi na kulinda uaminifu wa taaluma ya uandishi wa habari," amesema.

Amesema mwandishi atakayejitokeza kugombea nafasi za kisiasa iwapo atataka kurudi kwenye tasnia ya habari baada ya uchaguzi, anaweza kufanya hivyo kwa kuwa mwandishi wa makala maalum safu huku akiweka wazi katika makala yake kuwa aliwahi kugombea kupitia chama fulani cha siasa ambapo hatua hiyo itasaidia kulinda uwazi na kuzuia upotoshaji wa habari kwa wasomaji na taaluma ya uandishi wa habari ikabaki kuwa huru na yenye kuaminika.

Aidha kupitia mwongozo huo Baraza limevitaka vyama vya siasa kuzingatia majukumu yake ya kisiasa, kuviacha vyombo vya habari kuwa huru na kujiepusha kutumia vyombo vya habari kama njia ya kueneza propaganda zao bila kipingamizi.

Amesema pamoja na baadhi ya vyama vya siasa kuwa na vyombo vyake vya habari na kujitanabaisha na mtazamo wa vyama vya siasa, bado vyombo hivyo vya habari vina wajibu wa kuzingatia weledi na maadili pasipo kufanya propaganda za kuwachafua wengine ambao hawako kwenye chama ambacho chombo fulani cha habari kipo.

"Pia chombo hicho kisitumike kuwachafua wananchi au viongozi wa chama kingine ambacho, kipo tofauti na chama ambacho chombo hiki cha habari kinakipenda. Chombo hicho kisitumike kusema uongo kuhusu vyama vingine, na badala yake kiendelee kufuata maadili ya uandishi wa habari kwa kutoa haki sawa kwa vyama vyote" amesema.

Amesema kwa mujibu wa maadili ya uandishi, chombo cha habari kikisha jipambanua kuwa ni cha mlengo wa chama fulani, hakiruhusiwi kukandamiza upande mwingine, na badala yake kinajukumu la kufuata maadili kwa kuhakikisha vyama vingine pia vinapata nafasi kwenye chombo hicho.

Mbali ya waandishi wa habari na vyombo vya habari, baraza hilo pia limetoa mwongozo kwa taasisi za kihabari na kiraia, vyuo vya waandishi wa habari na mwongozo kwa makundi mbalimbali ikiwemo wanasiasa na maafisa wa Serikali, wafanyabiashara, wamiliki, wanahisa na wakurugenzi wa vyombo vya habari ambao wote wametakiwa kufuata na kuzingatia azimio la Dar es Salaam juu ya uhuru wa uhariri na uwajibikaji.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...