
Bodi Mpya ya Wakurugenzi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imekutana kwa mara ya kwanza na watumishi wa Taasisi hiyo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uwajibikaji, mshikamano na ufanisi katika kutimiza malengo yake ya msingi ya kuhifadhi na kusimamia mazingira nchini.
Mkutano huo umefanyika katika kikao cha kawaida cha kila mwezi cha watumishi, ambapo Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Mwanasha Tumbo, akiambatana na wajumbe wengine sita wa bodi, aliwasihi watumishi kuwa mstari wa mbele katika kuonesha mfano wa uadilifu, usafi wa mazingira, na utendaji wenye matokeo.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu uteuzi wa bodi hiyo, Mhandisi Mwanasha alisema:
“Ili tuweze kutimiza majukumu yetu ipasavyo kama Taasisi ya mazingira, lazima tuanze na sisi wenyewe – tuwe wasafi, wawazi, wenye upendo na tuwe tayari kusikiliza na kushughulikia changamoto za ndani kabla ya kwenda kwa wananchi.”
Amesisitiza kuwa utunzaji wa mazingira unaanzia, majumbani kwa Watoto wadogo na kisha kusambaa kwa jamii nzima. Alisema kuwa bodi itasimamia uwazi katika maamuzi, kushirikiana kwa karibu na menejimenti pamoja na kujenga mazingira bora ya kazi kwa watumishi wote.
“Kama kuna changamoto, zisemewe. Hakuna haja ya kuficha matatizo. Tuwe na utamaduni wa uwazi na kusaidiana kwa upendo. Hapo ndipo mafanikio yanapoanzia,” aliongeza.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, alipopata fursa ya kuzungumza aliikaribisha rasmi Bodi hiyo mpya na kueleza kuwa Menejimenti na watumishi wa NEMC wako tayari kushirikiana kwa dhati ili kuhakikisha taasisi inatekeleza wajibu wake kwa ufanisi.
“Tunawakaribisha kwa moyo wa dhati. Tumejipanga kushirikiana nanyi kwa karibu ili kuhakikisha dhamira ya NEMC ya kulinda na kusimamia mazingira ya Taifa letu inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa. Tuko tayari kwa mwelekeo mpya na tunawakaribisha kwa mikono miwili,” alisema Dkt. Semesi.
Kwa upande wao, watumishi wa NEMC walieleza matumaini yao mapya kwa uongozi wa bodi hiyo, wakisema kuwa hatua ya viongozi kukutana nao mapema ni ishara ya kuanzisha mahusiano ya karibu kati ya bodi na watendaji wa kila siku.
Bodi hiyo mpya ya Wakurugenzi ya NEMC inatarajiwa kuleta mwelekeo mpya wa kimkakati katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi, hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimazingira zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira na usimamizi wa taka.
















Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...