Kufuatia ziara yake yenye mafanikio jijini Dar es Salaam mwezi Juni mwaka huu, Mhe. Marianne Young, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, leo ameendelea na ziara yake kwa kutembelea kiwanda cha Bia cha Serengeti (SBL) kilichopo Moshi.

Ziara hii imeonesha uhusiano wa karibu wa kiuchumi kati ya Uingereza na Tanzania, huku ikisisitiza mchango mkubwa wa SBL kutoa ajira kwa Watanzania, uwezeshaji wa wakulima, maendeleo ya kilimo, na mapato ya serikali.

Uwepo wa Balozi huyo Moshi unaonesha upana wa shughuli za SBL, ikionesha jinsi kampuni hii inavyochangia kwa namna ya moja kwa moja katika kukuza uchumi wa mikoa na kuleta fursa za maendeleo kwa jamii mbalimbali.

Ziara hii imekuwa fursa ya kujifunza kwa undani zaidi kuhusu dhamira ya SBL ya kununua mazao ya ndani na kuwekeza katika jamii zinazozunguka maeneo ya viwanda vyake.

“Ni heshima kubwa kwetu sisi kama SBL kumpokea Mhe. Balozi Marianne Young hapa katika kiwanda chetu cha Moshi leo. Ziara hii ni uthibitisho wa ushirikiano thabiti kati ya Uingereza na Tanzania, na pia inatupa fursa ya kuonesha matokeo ya moja kwa moja ya uwekezaji wetu.

Hatujazalisha vinywaji tu, bali tunakuza maisha. Dhamira yetu ya kuwawezesha zaidi ya wakulima 600 wa ndani kupitia programu zetu za kununua mtama, mahindi na shayiri ikiwemo mpango wetu mpya wa 'Shamba ni Mali' ni kiini cha mkakati wetu.

Programu hizi, sambamba na jitihada zetu kupitia ‘Kilimo Viwanda’, zinatoa mafunzo muhimu, mbegu bora, na soko la uhakika, hivyo kuongeza kipato na kuinua maisha ya wakulima wetu,” alisema John Wanyancha, Mkurugenzi wa Mahusiano kwa Umma wa kampuni ya SBL.John aliongeza kuwa, “shughuli zetu hapa Moshi, Mwanza na Dar es Salaam zimekuwa chanzo cha ajira rasmi na zisizo rasmi kwa maelfu ya watu, huku mchango wetu mkubwa wa kodi ukiwa ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.”

Ziara hii ya Balozi katika kiwanda cha Moshi iliambatana na maelezo ya kina kuhusu mchakato wa utengenezaji wa bia, hatua za udhibiti wa ubora, pamoja na majadiliano kuhusu mustakabali wa kampuni ambao unategemea kwa kiasi kikubwa mazao ya kilimo ya ndani.

Ujumbe pia ulipata fursa ya kujifunza kuhusu mchango wa kiuchumi wa SBL, ikiwa ni pamoja na kuchangia pakubwa katika kodi kwa serikali ya Tanzania ambayo huchangia huduma muhimu za jamii na maendeleo ya miundombinu.

Mhe. Young alisema, “Ni jambo la kuvutia sana kushuhudia kwa macho yangu ukubwa na faida za shughuli za Kampuni ya Bia ya Serengeti hapa Moshi. SBL ni mfano wa jinsi uwekezaji wa kigeni unavyowajibika hasa kupitia kampuni inayomilikiwa na Diageo inavyoweza kuchochea maendeleo shirikishi ya kiuchumi.

Kuanzia utoaji wa ajira kwa maelfu ya Watanzania, kuwawezesha wakulima, hadi mchango wao mkubwa wa mapato kwa serikali, ni wazi kuwa SBL ni mdau muhimu katika mafanikio ya kiuchumi ya Tanzania.

Uingereza inajivunia kuunga mkono kampuni zinazochochea maendeleo endelevu na kushirikiana kwa dhati na jamii za ndani, hasa katika sekta ya kilimo.”

Ziara hii inaonesha maono ya pamoja kati ya Uingereza na Tanzania ya kujenga uchumi imara na jumuishi, unaojengwa juu ya misingi ya maendeleo endelevu na ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi na umma.

SBL inaendelea kuwa mfano wa biashara inayowajibika, ikithibitisha kuwa mafanikio ya kibiashara yanaweza kwenda sambamba na maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...