Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Global Education Link (GEL) imewataka wanafunzi wanaotaka kujiunga na vyuo vikuu kuwa makini na kozi wanazochagua wanapotaka kujiunga na vyyuo vikuu mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Ushauri huo ulitolewa jana na Meneja Mkuu wa GEL, Regina Lema, wakati wa maonesho ya kitaaluma ya vyuo vikuu mbalimbali kwa wanafunzi wa shule za sekondari zaidi ya 102 za Mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema GEL imekuwa ikitoa mwongozo kwa wanafunzi mbalimbali kuhusu kozi sahihi wanazopaswa kuchukua wanapokwenda kusoma vyuo vikuu mbalimbali na kwenye maonesho hayo wametoa elimu hiyo.

Regina alisema mbali na kutoa elimu hiyo, GEL imetoa huduma za udahili wa papo kwa papo, pamoja na ushauri wa taaluma na malezi ya kitaaluma kuwawezesha wanafunzi kuelewa vyema nini cha kusomea kwa ajili ya kufanikisha malengo ya Taifa ya mwaka 2025 hadi 2050.

Regina alisema kuwa kupitia ushiriki huo, GEL pia limeimarisha uhusiano wake na shule za msingi na sekondari kwa kushirikiana na walimu na wanafunzi waliotembelea mabanda yake.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, Albert Msando, alisema kuna umuhimu wa wanafunzi wakawekewa mazingira rafiki ya kuwa wabunifu na kufikiri ili hatimaye taifa liwe na kizazi chenye uwezo wa kufikiria kufanya mambo makubwa.

Maonesho hayo yaliyoandaliwa na Global Education Link (GEL), yanaendelea kwenye viwanja vya Mlimani City jijini ambapo maelfu ya wanafunzi wa shule za Dar es Salaam zinashiriki kupata mwongozo wa kusoma vyuo vikuu.

Msando alizipongeza taasisi zote zilizoshiriki kwenye maonesho hayo na kuongeza kuwa kuna umuhimu wa shule na taasisi za elimu kuonesha thamani ya elimu wanayotoa kwa vizazi vya sasa na vya baadae.

“Tusipokuwa na kizazi chenye elimu bora tutaendelea kusubiri sana, tukiwa na kizazi kisichokuwa bunifu tutabaki vile vile miaka nenda miaka rudi, tukiwa na kizazi kisichojua kufikiria tutaendelea kuwa watazamaji wakati wenzetu wanasonga mbele,” alisisitiza

“Elimu bora siyo anasa ni haki ya watoto nani wajibu wa watoa huduma ya elimu kutoa elimu bora na nimefurahi kuona watoto wadogo wanazungumza kichina hapa.

“Mimi sijui kichina lakini nimeona hapa watoto wanazungumza kichina kwa hiyo watanisaidia hata mimi siku nikipata wawekezaji wachina watakuwa wananitafsiria kwasababu bila hivyo wanaweza kuwa wanakusema wewe hujui,” alisema

“Hili ni jambo muhimu sana mmefanya ingawa eneo kama hili gharama ni kubwa kufanya maonesho kama haya lakini mkiandaa siku nyingine mtashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo na nitatoa maelekezo mpewe eneo bure la serikali kama Leaders Club na Tanganyika Packers,” alisema

Msando alisema kwenye mabanda aliyotembelea, amefurahia kuona vijana wakifanya vitu mbalimbali vya kitaaluma ambavyo vinaonyesha ni kwa kiasi gani vijana hao wanavipaji na wanaweza kufanya mambo makubwa kwa maendeleo ya taifa kama watalelewa vyema.

“Watoto wetu wanafundishwa kufikiria kwa hiyo wazazi na walimu lazima tuwasaidie tupate kizazi kinachofikiria. Taasisi za elimu ambazo nimeziona leo zinafanyakazi kubwa zinawaandaa watoto wetu kuweza kufikiria na kujiamini nawapongeza sana,” alisema

“Nimeona taasisi nyingi ikiwemo Global Education Link tujitahidi tufikishe huduma hizi kwenye ngazi za chini kabisa, kuna vijana wanaakili nyingi sana lakini wazazi wao hawajui watoto wao watasoma wapi, tutoke kwenye maorofa twende hadi ngazi ya mtaa tukawape maarifa ya wapi kwa kusoma,” alisema

Alizitaka taasisi za fedha kuingia makubaliano na wamiliki wa shule kuwapa mikopo nafuu kwaajili ya kuendesha shughuli zao za kila siku pale wazazi wanaochelewa kulipa ada kutokana na sababu mbalimbali.

“Kuna wakati mzazi anachelewa kulipa ada kutona na sababu mbalimbali kwa hiyo ili mwenye shule aweze kulipa mishahara ya wafanyakazi na gharama zingine za uendeshaji lazima apate mkopo nafuu kutoka kwenye benki ili kurahisisha shughuli zake za uendeshaji za kila siku,” alisema

“Shule binafsi zinaisaidia sana serikali hawa wote mnaowaona wanasoma shule binafsi zisingekuwepo hizi shule inamaana hawa wote wangekuwa kwenye shule za serikali kwa hiyo sekta binafsi inaisaidia serikali kwenye ukuaji wa elimu na utoaji wa huduma,” alisema Msando

Meneja Mkuu wa Global Education Link (GEL) Regina Lema, alisema maonesho yamekuwa na mafanikio makubwa sana kwani wanafunzi wengi wamehudhuria na wengine wamepata udahili wa papo kwa papo.

Alisema wamefanikiwa kuwapa mwongozo wa kozi za vyuo vikuu mbalimbali nje ya nchi wanafunzi wa shule zaidi ya 102 waliohudhuria

“Namshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kufika kwenye maonesho haya na kwa kutupa fursa ya kwenda kufanya maonesho kama haya mashuleni na tutaenda wilaya zingine za Dar es Salaam na mikoa mingine pia,” alisema

Regina alisema Global Education Link imekuwa ikipita kwenye shule mbalimbali kutoa mwongozo kwa wanafunzi kufahamu kozi zinazopatikana kwenye vyuo vikuu mbalimbali nje ya nchi na ufadhili unaotolewa na vyuo hivyo kupitia GEL.

“Pia katika maonesho haya tumefanya udahili wa papo kwa papo na pia hapa katika maonesho haya tunawawakilishi wa vyuo vikuu vya nje ya nchi kwenye mabanda yetu na tunatoa huduma zote ambazo ungezipata ofisini kwetu na kwenye ofisi zetu ambazo zimesambaa nchi nzima,” alisema











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...