Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua rasmi dawati maalum la kuwezesha biashara nchini (Trade Facilitation Desk) litakalokuwa na jukumu la kusimamia ustawi wa biashara kwa nchi nzima.
Uzinduzi huo umefanywa na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda katika Soko Kuu la Chifu Kingalu mjini Morogoro tarehe 16 Agosti 2025 ikiwa ni sehemu ya kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukuza sekta ya biashara nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa dawati hilo Bw. Mwenda amesema, dawati hilo, litaanza kufanya kazi rasmi tarehe 19 Agosti 2025, na litapatikana katika mikoa yote ya Tanzania, na madawati 200 tayari yameanzishwa nchi nzima.
“Lengo la dawati sio kukusanya kodi, bali ni kuwatambua wafanyabiashara, kuwasaidia kukua, na kutatua changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za kibiashara”, amesema Bw. Mwenda
Pia Bw. Mwenda amesisitiza kuwa, TRA ina nia ya dhati ya kushirikiana na wafanyabiashara ili kuimarisha uchumi wa taifa.
“Hili siyo dawati la kuwakamua wafanyabiashara bali ni la kuwasaidia kukua. Tunataka kuona kila mfanyabiashara akifanikisha ndoto zake za kibiashara,” amesema Bw. Mwenda
Aidha amesema kuwa dawati hilo litakuwa jukwaa la kupokea maoni na mapendekezo ya wafanyabiashara ili kuboresha mazingira ya kibiashara nchini.
Bw. Mwenda amesema kuwa, lengo lake ni kuona wafanyabiashara wakikua na kufanikisha biashara zao kwa kiwango cha juu.
Katika hatua ya kukuza biashara, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameelekeza kupunguzwa kwa kiwango cha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutoka asilimia 18 hadi asilimia 16 kwa wafanyabiashara wanaotumia mifumo ya kidijitali, kama vile malipo ya simu au benki.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Mkoa wa Morogoro, Bw. Ally Mamba, amepongeza hatua hiyo, akisema kuwa dawati hili litachangia pakubwa katika kustawisha sekta ya biashara nchini.
Vilevile, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wadogo Wadogo (Machinga) Mkoa wa Morogoro, Bw. Faustine Francis, ameonesha imani yake kuwa dawati hili litawasaidia wafanyabiashara wadogo kupata utambulisho rasmi na kuwasaidia kukua hadi kuwa wafanyabiashara wakubwa.
Uzinduzi huu unaashiria hatua muhimu katika juhudi za Serikali ya Tanzania za kukuza mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara, hasa wale wa sekta isiyo rasmi, na kuhakikisha wanapata nafasi ya kuchangia uchumi wa taifa kwa njia endelevu.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...