Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeendesha warsha kwa njia ya mtandao sambamba na mafunzo ya ana kwa ana kwa Wakufunzi wa Vituo vya Kufundishia wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi, ikiwa na lengo la kuwaongezea ujuzi na kuimarisha mbinu za ufundishaji.
Akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo kwa njia ya mtandao, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius A. Maneno, alisema mafunzo hayo yameandaliwa kwa ajili ya kuwakumbusha wakufunzi majukumu yao na kuhakikisha wanaendana na mitaala ya Bodi.
“Lengo letu ni kuona tunapandisha kiwango cha ufaulu kwa mitihani mbalimbali ya Bodi na kuongeza uelewa wa wanafunzi ili watakapomaliza wawe wabobezi katika masuala ya Uhasibu na Ukaguzi,” alisema Maneno.
Aidha, alitoa wito kwa Wakufunzi wa Vituo vya Kufundishia kuendesha baadhi ya masomo kwa njia ya mtandao, itasaidia kupunguza gharama za uendeshaji, kuwafikia wanafunzi wengi zaidi na pia kuendana na maendeleo ya teknolojia.
Naye Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu ya Taaluma na Mafunzo wa NBAA, Peter Lyimo, alisema Bodi hiyo imejipanga kuhakikisha wakufunzi wanapata nyenzo na ujuzi unaohitajika ili kuandaa watahiniwa ipasavyo, jambo litakalosaidia kila mtahiniwa kufanya mitihani vizuri na kuondoa changamoto zinazojitokeza mara kwa mara.
NBAA imekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha elimu ya Uhasibu na Ukaguzi nchini, kupitia programu mbalimbali za mafunzo na ushauri, ili kuhakikisha Taifa linapata wataalamu wenye weledi na kuaminika.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius A. Maneno akizungumza kwa njia ya mtandao wakati akifungua mafunzo kwa njia ya mtandao sambamba na mafunzo ya ana kwa ana kwa Wakufunzi wa Vituo vya Kufundishia wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu ya Taaluma na Mafunzo wa NBAA, Peter Lyimo akiwakaribisha wakufunzi waliofika kwa ajili ya kutoa mafunzo katika warsha ya ana kwa ana na kwa njia ya mtandao kwa Wakufunzi wa Vituo vya Kufundishia wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi.
Baadhi ya Wafanyakazi wa NBAA na Wakufunzi wa Vituo vya Kufundishia Wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi wakifuatilia mada pamoja na wale wanaofuatilia ana kwa ana na kwa njia ya mtandao kwa Wakufunzi wa Vituo vya Kufundishia wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...