
Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imepiga hatua kubwa leo kwa kukabidhi rasmi mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Huduma za Kibingwa kwa mkandarasi, ikiwa ni mwanzo wa safari ya kuboresha huduma za afya kwa wanajumuiya wa taasisi hiyo na jamii kwa ujumla.
Mradi huo, unaokadiriwa kugharimu shilingi bilioni 4.9, utalenga kutoa huduma maalumu za kitabibu kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya madaktari bingwa—ikiwa ni sehemu ya jitihada za NM-AIST kuchangia kwa vitendo maendeleo ya afya nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Makamu Mkuu wa Taasisi, Prof. Maulilio Kipanyula, alisisitiza dhamira ya NM-AIST kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa viwango vya juu na kukamilika kwa wakati.
“Tuna matarajio makubwa kwamba kituo hiki kitapunguza changamoto za upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa wanajumuiya wetu na wakazi wa maeneo ya jirani. Huu ni uwekezaji wa afya na maendeleo ya watu wetu,” alisema Prof. Kipanyula.
Mradi huo umekabidhiwa kwa Mhandisi Omar Kiure wa Kampuni ya Ujenzi ya Kiure, ambaye sasa ana jukumu la kuhakikisha ujenzi huo unatekelezwa kwa mujibu wa mkataba.
Aidha, Mwanamimari Ismail Mvungi, mshauri mshiriki wa mradi, aliungana na Mhandisi Wilhandrus Karumuna katika kuwasilisha eneo la ujenzi kwa mkandarasi, huku hatua hiyo ikionekana kama ishara ya mwanzo wa mabadiliko ya huduma za afya ndani ya NM-AIST.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha NM-AIST, Dkt. Michael Kileo, alisema:
“Kituo hiki kitakapokamilika, kitakuwa msaada mkubwa katika kutoa huduma za kibingwa kwa jamii, hasa kwa magonjwa ambayo kwa sasa hulazimu wagonjwa kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu.”
Ujenzi wa kituo hicho umegawanywa katika awamu kadhaa, ambapo awamu ya kwanza itagharimu shilingi bilioni 1.3 na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...