CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimeadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kwa kuzindua Kituo Kikubwa cha Umahiri cha Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji, hatua inayokiweka chuo hicho katika ramani ya vyuo bora vya sekta ya anga barani Afrika.
Sherehe hizo zimefanyika leo Agosti 21, 2025 jijini Dar es Salaam, zikihudhuriwa na viongozi wa kitaifa na wadau wa sekta ya uchukuzi, ambapo pia Mkutano wa tatu wa Kimataifa kuhusu Usafirishaji, Logistiki na Usimamizi katika Sekta ya Usafirishaji umefunguliwa rasmi.
Akizungumza katika uzunduzi huo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeipa sekta ya usafirishaji kipaumbele cha kipekee kwa kuiwezesha kuwa ya kisasa na salama, ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
“Sekta ya usafirishaji ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yoyote. Rais Samia ameweka kipaumbele kikubwa kwenye sekta hii na kielelezo kikubwa ni ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma. Hapo zamani tulitumia saa tisa kwa basi, leo tunatumia masaa matatu pekee kwa treni,” alisema Waziri Mbarawa.
Kwa mujibu wa Waziri, zaidi ya Sh bilioni 50 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya kuanzisha kituo hicho cha umahiri NIT, huku tafiti na mafunzo yanayofanyika chuoni hapo yakitarajiwa kusaidia kutatua changamoto za sekta ya uchukuzi
“Sekta ya usafirishaji ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yoyote. Rais Samia ameweka kipaumbele kikubwa kwenye sekta hii na kielelezo kikubwa ni ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma. Hapo zamani tulitumia saa tisa kwa basi, leo tunatumia masaa matatu pekee kwa treni,” amesema Profesa Mbarawa.
Amebainisha kuwa, Chuo cha NIT kimekua kutoka kuwa taasisi ndogo mwaka 1975 hadi kuwa moja ya vyuo vikubwa vya mfano Afrika Mashariki na Kati.
“Leo tunaanzisha kituo kikubwa cha umahiri ambapo Rais Samia amepeleka Sh bilioni 50 kwa ajili ya kuanzishwa kwake. Tafiti zinazofanyika NIT zikitekelezwa kwa vitendo zitasaidia kutatua changamoto nyingi katika sekta ya uchukuzi. Haitakuwa na maana kama tuna miundombinu ya kisasa bila wataalamu, ndiyo maana Serikali inaendelea kuwekeza kwenye vyuo vya sekta hii,” ameongeza Waziri.
Amesema Serikali pia imeanzisha kozi maalumu ya marubani nchini ili kupunguza gharama kubwa za kusomea nje, ambazo zilifikia kati ya Sh milioni 100 hadi 150, huku akibainisha kuwa mafunzo hayo sasa yanafundishwa hapa nchini kwa gharama nafuu lakini kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo NIT, Dkt. Prosper Mgaya amesema Chuo hicho kilianza kikiwa na wanafunzi 78 na sasa kina zaidi ya wanafunzi 17,000 wa kozi ndefu huku kila mwaka chuo kinatoa mafunzo kwa zaidi ya wanafunzi 10,000 wa kozi fupi.
“Sasa tuna vifaa vya kisasa na chuo chetu kinatambulika kimataifa. Tuna ithibati kutoka TCAA na pia ithibati inayotambulika na Umoja wa Ulaya. Hivyo, wahitimu wetu wanakubalika kimataifa,” amesema Mkuu wa NIT.
Amebainisha kuwa mojawapo ya matukio makubwa kwenye maadhimisho hayo ya miaka 50 ni uzinduzi wa Kituo cha Umahiri cha Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji, ambacho kimeingia makubaliano na taasisi mbalimbali za kimataifa kutoa mafunzo kwa wataalamu wa sekta hiyo.
“Tunafungua kampasi KIA kwa ajili ya mafunzo ya marubani ambapo mkandarasi tayari ameanza ujenzi, na pia tunafungua kampasi Lindi kwa ajili ya wataalamu wa usafiri majini. Haya ni maendeleo makubwa kwa NIT,” ameongeza.
Meneja wa Kampuni Tanzu ya NIT, Dkt. John Mahona amesema majukumu yao makuu ni kushirikiana na walimu wa chuo hicho katika kufanya ubunifu wa kiteknolojia ili Watanzania waweze kutengeneza magari na mitambo ya kisasa kwa manufaa ya taifa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...