Na Karama Kenyunko

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia Idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa imekutana na wadau mbalimbali mkoani Kigoma kwa ajili ya kutoa elimu juu ya mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Katika kikao hicho kilichofanyika Agosti 25, 2025, TRA imeeleza kuwa Serikali imepunguza kodi ya uingizaji wa vitenge kutoka asilimia 50 hadi asilimia 35, ili kuwahamasisha wafanyabiashara kutumia njia rasmi za Forodha badala ya magendo.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Ofisa Forodha Mkuu kutoka Makao Makuu ya TRA, Hassan Minga, amesema mabadiliko hayo yamelenga kusaidia wafanyabiashara wa vitenge, hususan Mkoa wa Kigoma, ambako biashara hiyo inapita kwa wingi kutoka nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

“Serikali bado inatoa wito kwa wafanyabiashara kutumia njia rasmi badala ya magendo, kwani kodi ya bidhaa ya vitenge imepunguzwa hadi asilimia 35. Hatua hii inalenga kufanya bidhaa hiyo ipatikane kwa unafuu kupitia njia halali,” amesema Minga.

Aidha, Minga amebainisha kuwa Serikali imefanya marekebisho kwenye kodi ya bidhaa nyingine ikiwemo saruji, ambapo tozo ya maendeleo ya viwanda (Industrial Development Levy) imeondolewa kwenye bidhaa ya saruji. Hatua hiyo inalenga kuwezesha kiwanda cha saruji kilichopo Kigoma kuagiza malighafi hiyo kutoka DRC na kupunguza gharama za uzalishaji.

Ameongeza kuwa Serikali pia imeendeleza unafuu wa kodi kwa viwanda vya chumvi ili kurahisisha upatikanaji wa malighafi na kupunguza gharama za chumvi ya mezani, hatua itakayoongeza ushindani wa bidhaa hiyo sokoni.

Kwa upande wake,Mohammed Mnonda, Meneja Msaidizi wa TRA Mkoa wa Kigoma kutoka Idara ya Forodha, amesema mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa wafanyabiashara na mawakala wa forodha, kwani yamewasaidia kuelewa mabadiliko ya kisheria na namna ya kuyatekeleza.

“Baada ya mafunzo haya, sisi kama watumishi wa forodha tutakuwa walimu wazuri wa kuwaelekeza wadau wengine. Tunatoa wito kwa wananchi wa Kigoma kufuata taratibu rasmi za forodha wanaposhusha au kuingiza mizigo nchini ili kuepuka usumbufu,” amesema Mnonda.

Naye Dunia Salutwe, wakala wa forodha aliyehudhuria mafunzo hayo, aliishukuru TRA kwa kuwaletea elimu hiyo, akibainisha kuwa mabadiliko hayo yamepunguza gharama kwa wafanyabiashara na kuhamasisha matumizi ya njia rasmi.

“Kupunguza ushuru wa vitenge na kuondoa kodi kwenye clinker kutasaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza mapato ya serikali kupitia forodha rasmi. Tunashauri TRA iendelee kutoa elimu mara kwa mara kwa wadau wa forodha ili kuongeza uelewa,” amesema Shakuru

Mabadiliko haya ya sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 yanatazamwa kama hatua muhimu ya kuimarisha biashara, kuongeza mapato ya serikali na kuwezesha mazingira bora ya uwekezaji hususan mkoani Kigoma, ambao ni lango kuu la biashara kati ya Tanzania na nchi jirani.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...