Mbinga - Ruvuma.
Katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi, TANESCO Mkoa wa Ruvuma imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya umeme kama nishati salama na rafiki wa mazingira kwa ajili ya kupikia.
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Msaidizi kutoka TANESCO Mkoa wa Ruvuma Emma Ulendo, ameongoza zoezi hilo la utoaji elimu kwenye banda la TANESCO, katika maadhimisho ya sikukuu ya Nanenane yanayofanyika eneo la Amani Makolo Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma.
Katika maelezo yake Emma amesema kuwa TANESCO inalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kuwaelimisha kuhusu faida za matumizi ya umeme majumbani, hasa kwa kupikia, hatua inayosaidia kupunguza matumizi ya mkaa na kuni ambazo ni hatari kwa afya na mazingira.
Aidha Emma ameeleza kuwa TANESCO inatumia fursa hiyo kuwafahamisha wananchi kuhusu taratibu za kuunganishiwa umeme pamoja na gharama zake, ili kila mwananchi awe na uelewa sahihi wa mchakato mzima.
Wananchi pia wanaendelea kupatiwa elimu kuhusu huduma za kidijitali zinazotolewa na TANESCO kama vile malipo kwa njia ya mtandao, kuwasiliana kupitia mitandao ya kijamii, pamoja na namba ya huduma kwa wateja isiyolipiwa 180, ambayo inaweza kupigwa muda wowote kwa ajili ya msaada au taarifa yoyote muhimu.
Maonesho ya Nanenane yamekuwa jukwaa muhimu kwa taasisi kama TANESCO kufikisha elimu kwa wananchi juu ya huduma mbalimbali, huku yakihimiza matumizi ya teknolojia na nishati safi ili kujenga jamii yenye maendeleo endelevu.
Maonesho ya Nanenane yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Amani Makolo, Mbinga yalifunguliwa rasmi jana, tarehe 3 Agosti, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, maonyesho hayo yanatarajiwa kufungwa tarehe 10 Agosti mwaka 2025.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...