Dodoma, Agosti 4, 2025

Tume ya Madini kwa kushirikiana na taasisi nyingine chini ya Wizara ya Madini, inashiriki kikamilifu kwenye Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Uwepo wa Tume katika maonesho haya unalenga kuonesha fursa lukuki zilizopo katika sekta ya madini nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na utafiti wa madini, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini.

Katika banda lake la maonesho, Tume ya Madini imevutia idadi kubwa ya wananchi wanaotaka kujifunza namna sekta ya madini inavyotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa. Wataalam wa Tume wameeleza jinsi Tanzania inavyojipanga kuwa kitovu cha uchimbaji endelevu wa madini na kuongeza thamani kwa bara la Afrika, huku wakieleza sera, mifumo na fursa mbalimbali zilizowekwa ili kuwawezesha wawekezaji na wananchi kushiriki kikamilifu.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Meneja wa Mahusiano kwa Umma na Mawasiliano wa Tume ya Madini, Greyson Mwase, amesema kuwa lengo kuu la ushiriki wa Tume katika maonesho haya ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna wanavyoweza kushiriki moja kwa moja katika sekta ya madini na kunufaika nayo kiuchumi.

“Tunataka wananchi waelewe kuwa sekta ya madini si kwa wawekezaji wakubwa tu. Kuna nafasi kubwa kwa wachimbaji wadogo, wajasiriamali, na vijana wenye taaluma mbalimbali kushiriki kupitia uchimbaji mdogo, uchenjuaji, biashara ya madini, na utoaji wa bidhaa na huduma kwenye migodi,” amesema Mwase.

Ameongeza kuwa Tume inawahimiza wananchi kutuma maombi ya Leseni za Uchimbaji Mdogo wa Madini (PMLs), kuanzisha viwanda vidogo vya kukata na kung’arisha madini (lapidaries), pamoja na kuyeyusha madini kama dhahabu, vito vya thamani, na madini ya viwandani.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wadau wa madini kutumia masoko na vituo vya ununuzi wa madini vilivyoanzishwa nchini ili kunufaika kwa kuuza madini yao kulingana na bei elekezi inayotolewa na Tume kila siku kwa kuendana na Soko la Dunia.

Kuhusu ushiriki wa Watanzania katika utoaji wa huduma kwenye migodi, Mwase amesema Tume inatekeleza Kanuni za Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini ambazo zinahamasisha kampuni za madini kuajiri Watanzania, kununua bidhaa na huduma ndani ya nchi, na kusaidia katika uhamishaji wa ujuzi.

“Huduma kama upishi, usafirishaji, usambazaji wa mafuta, ujenzi, na ulinzi ni maeneo ambayo Watanzania wengi wanaweza kuyatumia kupata kipato kupitia sekta hii. Tume inawahimiza wasajili biashara zao, wapate vyeti vinavyotakiwa, na waongeze uwezo wao wa kiufundi,” amesema.

Amesisitiza pia kuwa vijana wa kitanzania wanayo nafasi kubwa ya ajira na ujasiriamali kwenye sekta ya madini, hasa kwa wale wenye taaluma katika sayansi, uhandisi, uhasibu, mazingira, mawasiliano na uendeshaji wa mitambo.

Maonesho ya Nane Nane yataendelea hadi tarehe 8 Agosti 2025. Wananchi wote wanakaribishwa kutembelea banda la Tume ya Madini ili kupata elimu kutoka kwa wataalam wa sekta hiyo, kupata machapisho ya elimu, na kubaini fursa mbalimbali za kushiriki na kunufaika na sekta ya madini inayokua kwa kasi nchini Tanzania.






Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...