SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka waokaji wa mikate nchini kuhakikisha wanazingatia viwango vya ubora na usalama wa chakula ili kulinda afya za watumiaji na kukuza masoko ya bidhaa zao.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa TBS, Mhandisi Abdallah Kileo, wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa waokaji yaliyofanyika katika ofisi za shirika hilo, eneo la Ubungo.

Mhandisi Kileo alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo waokaji kuhusu umuhimu wa kufuata viwango vya ubora vinavyotambulika kisheria, ili kuepusha madhara kwa walaji na kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinakubalika ndani na nje ya nchi.

“Kupitia wawakilishi waliopo hapa, tunatarajia elimu hii itawafikia hadi waokaji waliopo mitaani. Tunawahimiza waokaji wote ambao bado hawajathibitisha bidhaa zao waje wapate mafunzo,” alisema.

Aliongeza kuwa waokaji wasiothibitisha ubora wa bidhaa zao hukosa fursa za soko na hukabiliwa na hatari ya kufungiwa uzalishaji pindi wanapokiuka sheria za usalama wa chakula.

“Matumizi ya nembo ya TBS ni muhimu kwa bidhaa kutambulika na kukubalika kitaifa na kimataifa. Hii ni kwa faida ya kiuchumi na afya ya mlaji,” alisisitiza Mhandisi Kileo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Waokaji Tanzania (TBA), Bi. Fransinca Lyimo, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita na TBS kwa kuratibu mafunzo hayo, akisema ni hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya uokaji nchini.

“Kupitia mafunzo haya, waokaji watajifunza wajibu wao, kanuni za usalama wa chakula, na kuongeza ubora wa bidhaa, jambo ambalo lina faida kwa walaji na kwa uchumi wa taifa,” alisema.

Naye mmoja wa waokaji walioshiriki mafunzo hayo, Bi. Ashura Bendera, alisema elimu aliyopata itamsaidia kuboresha biashara yake na kufikia viwango vya soko la ushindani.

“Nitayatumia mafunzo haya kubadilisha biashara yangu. Nimejifunza mengi kuhusu ubora na usalama wa bidhaa,” alisema Ashura.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za TBS kuhakikisha bidhaa zote za chakula nchini zinazingatia viwango vya kitaifa na kimataifa kwa ajili ya afya ya walaji na ushindani wa kibiashara.













Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...