*Asema  itakuwa na gati za kisasa na ndefu ambazo zitakuwa na uwezo kupokea meli kubwa 

*Asisitiza bandari hiyo itajengwa sambamba na eneo maalum la kiuchumi hekta 9800

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Pwani

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema iwapo Chama hicho kitapata ridhaa ya kuwatumikia Watanzania kitakwenda kujenga bandari ya Bagamoyo katika eneo la Mbegani mkoani Pwani.

Akihutubia maelfu ya wananchi wa Kibaha mkoani Pwani katika mikutano ya kampeni kuomba kura kuelekea Oktoba 29,2025 Dk. Samia ametumia mkutano huo kuelezea mipango ya Serikali katika miaka mitano ijayo.

Ambapo amesema kuwa mapema mwaka huu alihudhuria katika Mkoa huo kwa ajili ya kuzindua bandari kavu ya Kwala ambao uliendana na historia ya uzinduzi wa safari za treni ya mizigo kwa njia ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.

Amesema kuwa lengo ni kuona sehemu kubwa ya mizigo inayopita Bandari ya Dar es Salaam inapelekwa  moja kwa moja Kwala kisha magari ya mizigo yatashusha na kupakia mizigo eneo hilo.

Dk.Samia pia amesema mradi mwingine wa kihistoria ni Bandari ya Bagamoyo ambao umesubiriwa kwa muda mrefu lakini wakipata ya kuongoza nchi watakwenda kuijenga Bandari ya Bagamoyo katika eneo la Mbegani.

"Bandari hiyo itakuwa na gati za kisasa na ndefu ambazo zitakuwa na uwezo kupokea meli kubwa zaidi kuliko Bandari ya Dar es Salaam.Bandari hiyo itaunganishwa kwa reli ya SGR kwa kipande cha kilometa 100 kutoka Bandari kavu ya Kwala hadi Bandari ya Bagamoyo.

Ameongeza kwamba bandari hiyo itajengwa sambamba na eneo maalum la kiuchumi hekta 9800 litakalochochea na kuvutia uwekezaji wa viwanda.”Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi na andiko la biashara.”

"Tunakwenda kutekeleza mradi huu kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania, Shirika la Reli Tanzania, sekta binafsi hususan ujenzi wa kongani za viwanda.

Aliongeza: "Hii ni miradi ya kimapinduzi kuweza kufanyika ndani ya Mkoa wa Pwani kuwa kitovu cha usafirishaji nchini, kujenga fursa za ajira na biashara kwa wananchi lakini Tanzania kwa ujumla."

"Imani yetu ni kusimamia na kuendeleza miradi hii muhimu kwa maendeleo yetu na nchi kwa ujumla," alisisitiza.

Kwa upande mwingine ,Mgombea Urais Dk.Samia amesema  mkoa huo unastahili pongezi kwa kasi kubwa ya maendeleo ya viwanda ambapo idadi imeongezeka kutoka viwanda 1,587 hadi viwanda 1,631 kwa mwaka huu.

Amefafanua ongezeko hilo sawa na ongezeko la viwanda 244 ndani ya miaka minne au viwanda 61 kila mwaka.

Amesema viwanda vya kati 81 vimejengwa ambapo sasa vimefikia 161 sawa na viwanda 26 kila mwaka."Viwanda hivi vimetoa ajira za moja kwa moja 21,146 na zisizokuwa za moja kwa moja ajira 60,000…

“Hapa sijavitaja viwanda vidogo ambavyo vimewanufaisha Watanzania wengi kwa bidhaa zinazozalishwa nchini.Uwekezaji uliofanyika umewezesha nchi yetu kupiga hatua kujitegemea kimapato na bidhaa.

“Kwa mfano  ndani ya Mkoa wa Pwani kuna uzalishaji mkubwa unaofanya nchi ijitegemee kwenye bidhaa muhimu.”Sasa tunajitegemea kwenye uzalishaji vioo lakini marumaru, saruji, mabati ya rangi vyote vinazalishwa ndanibya nchi."

Pia Dk. Samia amesema  kutokana na kasi kubwa ya ukuaji viwanda serikali imeamua kujenga vituo vya kupoza umeme eneo la Msufini Mkuranga kwa gharama ya sh. bilioni 388.3.

“Kituo kingine kitajengwa Zegereni Kibaha kwa gharama ya sh. bilioni 54.7 na Zinga Bagamoyo kwa sh. bilioni 120.Umeme huo utakuwa wenye uhakika kuufanya mkoa huo kutokumbwa na upungufu wa umeme, hivyo viwanda vitazalisha muda wote.

Dk. Samia amesema kwamba  endapo CCM ikipewa ridhaa serikali yake imejipanga kujenga mtandao wa gesi kutoka Kinyerezi hadi Chalinze ambayo itakuwa na matoleo kuelekea maeneo ya uwekezaji ya TAMCO, Zegereni, Kwala na Bagamoyo.

“ Kwasasa mkandarasi mshauri anaendelea kufanya tathimini ya njia ya kupitisha bomba hilo.Ujio wa gesi utazidi kuvutia uwekezaji mkoani Pwani kwani viwanda vitaendeshwa kwa gharama nafuu zaidi na bidhaa zitakazozalishwa vitapungua bei.

Dk. Samia amesema miongoni mwa ahadi katika ilani ya CCM ni kuchukua hatua kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi nchini kuwezesha wananchi wa kipato cha chini kujenga nyumba bora za kisasa kwa gharama nafuu.

Amebainisha mwelekeo wa serikali ni kuendeleza mpango wa ujenzi makazi bora kwa bei nafuu.”Serikali yake itaendelea kuboresha makazi mijini kwa kuhakikisha makazi, nyumba na majengo yote yanarasimishwa kwa kupimwa, kupangwa na kumilikishwa.”










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...