*Yamefanyika mengi miaka mitano iliyopita na tutafanya mengi zaidi 

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Mtwara

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.Samia Suluhu Hassan ameendelea kuchanja mbuga kusaka kura za urais katika Uchaguzi mkuu mwaka huu ambapo leo Septemba 23,2025 amepokelewa na maelfu ya wananchi Wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara akitokea mkoani Ruvuma.

Dk.Samia Suluhu Hassan akiwa katika mkutano uliofanyika eneo la Makanga wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara amesema CCM itashinda  katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29,2025.

“Ahsante sana wananchi wa Nanyumbu kwa mapokezi haya kwani mmejtokeza kwa wingi,hodi Mtwara na hakika mmenipokea kwa mikono miwili.Nasema ahsanteni sana…leo ndugu zetu wa Ruvuma wananifanyia Send off ya kuja Mtwara.

"Ushindi tutashinda Chama Cha Mapinduzi, maendeleo yanayojitokeza na yaliyofanyika bila shaka tutashinda. Tunataka ushindi wa heshima wa kuwafunga midomo wale wengine.

"Tunataka ushindi wa heshima, kwa hiyo tarehe 29 mwezi wa 10 tunaomba kura kwa Chama Cha Mapinduzi kwa mafiga matatu.Kwa pamoja tunakuja kujenga Taifa letu.

“Hii ni imani yenu kwa Chama Cha Mapinduzi kwa viongozi wenu ambao kwa pamoja tumefanyakazi kulijenga taifa letu," amesema Dk.Samia huku akieleza kuwa amefika katika Mkoa huo kwa kazi moja tu ya kuomba kura baada ya kutimiza miaka mitano ya kwanza.

"Sasa tunarudi tena kuomba kura kwa kujiamini kamba chama cha mapinduzi, serikali zake ndizo zinazoweza kufanyakazi ya kuinua hali na utu wa Mtanzania.

"Tumefanya miaka mitano iliyopita, tunaimani na tunajiamini kwamba tunaweza kufanya miaka mitano inayokuja. Na ndiyo maana tunaomba kura," amesema Dk.Samia.

Akieleza zaidi pia amesema mengi yamefanyika katika miaka mitano iliyopita katika Wilaya ya Nanyumbu kuanzia shule za msingi na sekondari, vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya, maji, umeme vyote wananchi wameshuhudia.

Kuhusu nishati ya umeme amesema Serikali  inatekeleza mradi wa gridi imara wenye thamani ya sh. bilioni 300.7 ambao itajengwa njia ya kusafirishia umeme kutoka Songea hadi Tunduru kisha Masasi.

Pia amesema Serikali itajenga vituo viwili vya kupoza umeme kimoja Tunduru ambacho kimefikia asilimia 50 na kingine Masasi."Lengo la vituo hivyo ni kuhakikisha Mtwara inapata umeme wakati wote bila kukatika au kupungua nguvu," alieleza.

Akizungumzia ujenzi wa barabara katika Mji wa Mangaka aliwaahidi wananchi kwamba serikali itaimarisha barabara za lami katika mji huo na mitaa yake.

Pia amesema kwamba  serikali itaendelea kujenga barabara zinazounganisha wilaya na makao makuu ya mkoa kwa kiwango cha changarawe na lami ziweze kupitia kipindi chote.

Dk. Samia alisema anatambua changamoto ya wanyamapori waharibifu ambao wanaharibu mashamba na wakati mwingine kujeruhi wananchi.

"Hasa kwa wale waliozungukwa na Pori la Akiba Lukwira na Lumesule ambapo wanyama hao wamekuwa wakiharibu mazao.

"Tatizo tunalijua, tunakwenda kuchukua jitihada za makusudi kuhakikisha wanyama hao wanabaki katika maeneo yao na hawaji kwenye maeneo ya wananchi," amesema Dk.Samia Suluhu Hassan.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...