NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
BENKI ya Equity Tanzania imewahakikishia wafanyabiashara wa soko la kimataifa Kariakoo mikopo ya kidijitali yenye riba nafuu, hatua itakayosaidia kuimarisha mtaji na kukuza biashara zao ndani na nje ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 10, 2025 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Biashara wa benki hiyo, Bw. Prosper Nambaya, aliyemwakilisha Mtendaji Mkuu wa Equity katika Kongamano la Umoja wa Wafanyabiashara wa Kariakoo.
Nambaya amesema benki hiyo ina mtaji mkubwa unaofikia zaidi ya trilioni 4 za Kitanzania, mtaji ambao una uwezo wa kufadhili sekta mbalimbali za biashara zikiwemo ujenzi na huduma za kimataifa.
“Equity inatoa mikopo ya kidijitali yenye riba ndogo kwa wafanyabiashara (Digital Lending). Kupitia upembezi yakinifu, benki hubaini kiwango cha mkopo kwa mteja wake bila kumlazimisha kuwa na fedha mkononi wakati wa manunuzi,” amesema Nambaya.
Aidha amesema kuwa kupitia kongamano hilo, wafanyabiashara wameelimishwa namna ya kufanya miamala ya kifedha hata wakiwa nje ya nchi, jambo litakalorahisisha usafirishaji na ufanyaji wa biashara kimataifa.
Pamoja na hayo amebainisha kuwa Benki ya Equity imejikita katika nchi sita za Afrika Mashariki ambazo ni Kenya, Tanzania, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Ethiopia, na inaendelea kupanua huduma zake ili kuwafikia wajasiriamali zaidi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Bw. Severine Mushi, ameipongeza Equity Bank kwa elimu waliyoitoa, akisema imetoa fursa kwa wafanyabiashara kuchagua huduma mbalimbali ikiwemo mikopo, bima na huduma za dola.
Mushi amekumbusha changamoto za miaka mitatu iliyopita ambapo biashara zilidorora na taasisi za kifedha kusita kutoa mikopo kutokana na mazingira magumu ya ukusanyaji kodi.
“Kabla ya mwaka 2022 biashara zilikuwa ngumu. Sheria za kodi hazikuwa rafiki, wengi walifilisika na hata benki zikawa na mashaka kutoa mikopo. Lakini baada ya serikali kurekebisha baadhi ya mambo, biashara zikaanza kurejea na hali sasa inaimarika,” amesema.
Naye mfanyabiashara wa vipodozi ambaye pia ni mshiriki wa kongamano hilo, Bi. Ghati Marwa amesema kuwa mikopo ya haraka kutoka Equity Bank imekuwa msaada mkubwa katika shughuli zake, hasa wakati wa kutoa mizigo bandarini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...