Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA)  imeendesha warsha ya siku nne kuhusu uandaaji wa muongozo  na ripoti kuhusu masuala ya Taarifa endelevu ''Sustainabiliy Reporting" ili kusaidia serikali katika juhudi za kufikia malengo ya maendeleo endelevu 2030 (SDG 2030). Taarifa hizo zitazingatia kuripoti maendeleo endelevu (IFRS S1) na Uwazi katika kuripoti athari za kwenye mazingira (IFRS S2).

Warsha hiyo inafanyika kuanzia Septemba 16 hadi 19, 2025, ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta mbalimbali kuelewa na kutekeleza viwango hivyo kwa ufanisi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius A. Maneno, alisema utekelezaji na uwasilishaji wa taarifa endelevu ni hatua muhimu kwa Taifa katika kuimarisha uwajibikaji wa kifedha, kijamii na kimazingira.

“Ripoti za kifedha sasa hazitahusisha hesabu pekee, bali zitajumuisha taarifa zinazohusu mazingira, jamii na utawala bora. Hii itasaidia kuhakikisha taasisi zote zinachangia kikamilifu katika maendeleo endelevu ya taifa letu na dunia kwa ujumla,” alisema CPA Maneno.

Aidha, alibainisha kuwa NBAA tayari imeanza rasmi utekelezaji wa Viwango vya Kimataifa vya Taarifa endelevu (IFRS S1 na S2) kufuatia kuidhinishwa kwa viwango hivyo katika kikao cha 102 cha Bodi kilichofanyika Septemba 2023. Viwango hivyo vilizinduliwa rasmi Oktoba 18, 2023 jijini Dodoma na vimeanza kutumika rasmi nchini kuanzia Januari 2024.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dkt. Germana Leyna alisema mafunzo haya yamekuja kwa wakati muafaka, hasa kwa Taasisi zinazotekeleza majukumu yenye mchango wa moja kwa moja katika maendeleo endelevu.

“Kumekuwa na changamoto ya uelewa mdogo kuhusu dhana ya maendeleo endelevu katika taasisi nyingi. Mafunzo haya yanatusaidia kuelewa jinsi ya kutafsiri majukumu yetu katika mifumo na sera za Taasisi ili kuhakikisha utekelezaji wa viwango hivi unafanyika kwa weledi,” alisema Dkt. Leyna.

Aliongeza kuwa kupitia warsha hiyo, sasa taasisi zitakuwa na kipimo rasmi na mfumo mahsusi wa kupima uwajibikaji wao katika muktadha wa Mazingira, Jamii na Utawala Bora; "Enviromental, Social and Good Governance" (ESG)

Warsha hii imewakutanisha washiriki kutoka sekta ya umma na binafsi wakiwemo wawakilishi kutoka mashirika ya kifedha, makampuni makubwa, taasisi za serikali na wasimamizi wa sekta mbalimbali. 

Kupitia warsha hii, NBAA inalenga kuimarisha mabadiliko chanya katika utayarishaji wa taarifa za fedha zenye kuzingatia maendeleo endelevu.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius A. Maneno akisoma hotuba ya ufunguzi wa warsha ya siku nne ya uandaaji wa muongozo  na ripoti kuhusu masuala ya Taarifa endelevu ''Sustainabiliy Reporting" inayofanyika katika ukumbi wa APC Bunju jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 16 hadi 19, 2025 .





Baadhi ya washiriki wa warsha kutoka taasisi za umma na Binafsi wakifuatilia hotuba ya Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius A. Maneno wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku nne ya uandaaji wa muongozo  na ripoti kuhusu masuala ya Taarifa endelevu ''Sustainabiliy Reporting"
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius A. Maneno  akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa NBAA pamoja na washiriki wa warsha kutoka taasisi za umma na Binafsi wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku nne ya uandaaji wa muongozo  na ripoti kuhusu masuala ya Taarifa endelevu ''Sustainabiliy Reporting"

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...