Na Mwandishi wetu Dodoma

Katika juhudi za kuimarisha mshikamano kazini na kuinua morali ya utendaji kazi kwa watumishi wake, Benki ya CRDB imezindua msimu wa tano wa mashindano ya CRDB International Supa Cup, ambapo kwa mara ya kwanza mashindano hayo yamevuka mipaka ya nchi kwa kuzikutanisha timu kutoka mataifa jirani.

Uzinduzi huo umefanyika leo, Oktoba 19, 2025, jijini Dodoma, ukiongozwa na Mkurugenzi wa Oparesheni wa CRDB, Admini Mwansansu, na kuhudhuriwa na wafanyakazi kutoka matawi mbalimbali ya ndani na nje ya Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwansansu alisema kuwa mashindano hayo yatafanyika kwa muda wa siku tano, yakihusisha michezo mbalimbali inayolenga si tu kuburudisha, bali pia kuhimiza afya na mshikamano miongoni mwa wafanyakazi.

“Kupitia mashindano haya, tunalenga kujenga afya njema kwa watumishi wetu, kuimarisha mshikamano wa kiutendaji na kuinua morali kazini. Mwisho wa siku haya yote yanaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wateja wetu,” alisema Mwansansu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa benki hiyo, Timothy Fasha, alisema kuwa mashindano hayo si tu uwanja wa michezo, bali pia jukwaa la kukuza mawasiliano ya ndani na kuimarisha ari ya pamoja katika kufanikisha malengo ya taasisi.

“Mashindano haya yanasaidia sana kujenga umoja miongoni mwa watumishi wetu. Ni fursa ya kipekee ya kuungana nje ya mazingira ya kazi na kujifunza kutoka kwa wenzao, jambo linalosaidia hata katika utoaji wa huduma bora kwa wateja,” alisema Fasha.

Wafanyakazi nao hawakusita kueleza furaha yao. Sela Benson, mtumishi kutoka CRDB Namanga, alisema kuwa ushiriki wa timu kutoka mataifa jirani umeleta msisimko mpya na kuwapa fursa ya kujifunza tamaduni tofauti huku wakiburudika na kushindana kwa amani.

“Ni jambo la kufurahisha sana kuona tunashindana na wenzetu kutoka nje ya Tanzania. Tunajifunza mengi kupitia michezo, tunatengeneza urafiki mpya, na zaidi tunajenga mshikamano ambao hatuwezi kuupata mezani kazini,” alisema Sela kwa furaha.


Mashindano hayo, ambayo sasa yamegeuka kuwa sehemu muhimu ya utamaduni wa ndani wa benki hiyo, yanatarajiwa kuhitimishwa wiki hii kwa fainali kubwa, huku timu mbalimbali zikitarajiwa kupambana kuwania ubingwa wa mwaka huu.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...