HANDENI TC
Halmashauri ya Mji wa Handeni imefanya bonanza kubwa la michezo lililolenga kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Bonanza hilo limefanyika leo katika Uwanja wa Kigoda, Handeni, na limehusisha wananchi, watumishi wa umma, viongozi wa dini, viongozi wa kisiasa na taasisi binafsi.
Akizungumza katika bonanza hilo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, amewataka wananchi wote waliojiandikisha kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kupiga kura ili kutimiza haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka.
“Nawasihi wananchi wote wa Handeni kujitokeza mapema siku ya uchaguzi. Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni. Serikali imeimarisha ulinzi na usalama, hivyo kila mmoja atapiga kura kwa amani na utulivu kama tulivyoshiriki bonanza letu leo,” amesema Mhe. Nyamwese.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni, Maryam Ukwaju, amewahimiza watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla kuendeleza ushirikiano na mshikamano kupitia michezo, akibainisha kuwa michezo ni chachu ya umoja na afya bora.
Bonanza hilo lilihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, kukimbia, kuvuta kamba, na mbio za taratibu.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...