MAHAKAMA Kuu, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, inatarajiwa Oktoba 13, mwaka huu kutoa uamuzi mdogo kuhusu pingamizi lililowasilishwa na upande wa Jamhuri, juu ya maelezo ya shahidi ambayo upande wa utetezi uliomba yapokelewe na mahakama ili mshitakiwa ayatumie katika maswali ya dodoso.

Mshitakiwa katika shauri hilo ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini ambayo ipo katika hatua ya usikilizwaji.

Hatua hiyo imefikiwa Leo Oktoba 10,2025 mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiana na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Awali, Lissu alianza kumhoji Mkaguzi wa Polisi kutoka Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandao, PF 22863 John Kaaya (45), ambaye alikuwa ametoa ushahidi wake wa msingi hapo jana.

Katika maswali yake ya awali, Lissu alimuuliza shahidi huyo ikiwa anauelewa kuhusu tume mbalimbali zilizowahi kuundwa kwa ajili ya mabadiliko ya Katiba, zikiwemo zile zilizokuwa chini ya majaji Francis Nyalali, Robert Kisanga, Mark Bomani na Joseph Warioba, katika vipindi tofauti vya uongozi.

Akijibu, Kaaya alisema hakumbuki tume nyingine kwa kuwa nyingi ziliundwa miaka mingi iliyopita wakati yeye bado yuko shule, lakini alikiri kuifahamu Tume ya Warioba, ambayo iliundwa wakati wa Awamu ya Nne ya Uongozi na rasimu yake kujadiliwa bungeni kwa muda wa miezi sita.

Baada ya maswali hayo, Lissu alimuuliza Kaaya kama aliwahi kuandika maelezo yoyote kabla ya kutoa ushahidi wake mahakamani, na shahidi akajibu kwamba alifanya hivyo na angeweza kuyatambua akiyaona.

Lissu alichukua nakala ya maelezo hayo, akaisoma na kisha kudai kwamba alibaini vipengele 47 vilivyokuwa vinakinzana kati ya ushahidi aliotoa mahakamani na maelezo aliyoyatoa awali. Alidai kuwa kabla ya kuendelea na maswali ya dodoso, mahakama inapaswa kupokea maelezo hayo kama kielelezo.

Akirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika kesi ya Lilian Jesus Fotes ya Septemba 2, 2020, Lissu alisema msingi wa hoja yake unatokana na kanuni kwamba shahidi hawezi kuulizwa maswali ya dodoso kabla ya maelezo yake kupokelewa rasmi.

Baada ya maombi hayo, upande wa Jamhuri ulipinga vikali hoja hizo.

Wakili wa Serikali Mkuu, Ajuaye Zegeli, aliibua pingamizi akidai kuwa Lissu hajafuata utaratibu unaotakiwa kisheria, akibainisha kuwa lengo la maelezo ya shahidi ni kuonyesha mkinzano wa kile alichokisema mahakamani na alichokiandika, si kuonyesha mambo aliyoyaacha.

Naye Wakili wa Serikali Mkuu, Ignus Mwiinuka, alidai mshtakiwa hakuzingatia ipasavyo kanuni za msingi za kumhoji shahidi kuhusu uaminifu wake. Alisema upande wa Jamhuri hauna tatizo na Lissu kusoma maelezo kwa shahidi, lakini taratibu nyingine hazikuzingatiwa.

“Anayepaswa kutoa maelezo haya kuwa kielelezo ni shahidi, si mshtakiwa. Hatujasikia mshtakiwa akimuuliza shahidi kama anataka kuyatoa. Badala yake, mshtakiwa mwenyewe ndiye ameomba mahakama yapokee,” alisisitiza Mwiinuka.

Akijibu hoja hizo, Lissu alisisitiza kuwa msimamo wa Mahakama ya Rufani ni wazi kwamba huwezi kumdodosa shahidi kabla ya maelezo yake kupokewa kama kielelezo, akieleza kuwa amefuata utaratibu sahihi.

“Waheshimiwa majaji, nimefuata utaratibu. Wameniletea rejeo la uamuzi. Siku ile nilikosea kwa kuwa sikuwa na rejeo hilo, lakini leo nimezingatia kila hatua. Naombeni msikubali pingamizi hili,” alisema Lissu.

Hata hivyo, Wakili Mwiinuka na Zegeli walisema kuwa baada ya kusikiliza hoja za mshtakiwa, bado msimamo wao ni kwamba utaratibu haukuzingatiwa ipasavyo.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama iliahirisha shauri hilo hadi Oktoba 13, mwaka huu saa 3:00 asubuhi, kwa ajili ya kutolewa kwa uamuzi mdogo kuhusu pingamizi hilo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...