WAKATI Watanzania wakijiandaa kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu jamii ya Rastafali nchini Tanzania wamesema ni vema zikapigwa kura za ushindi wa kishindo wenye kuashiria amani na upendo kwa ajili ya urithi wa vizazi vya Taifa hili.
Jamii hiyo ambayo inaamini kwa kiongozi wao wanamuita Jah huku Mfalme wa zamani wa Ethiopia, Haile Selassie, wakimpa umuhimu wa pekee. Marasta wengi humuona kama mwili wa Jah duniani na kama ujio wa pili wa Yesu Kristo.
Akizungumza na Michuzi TV na Michuzi Blog leo Oktoba 27,2025, jijini Mwanza Mfalme Valelian Bagaile Kuwani Mkuu wa Imani ya Rastafali Tanzania amesema iwapo zikitokea vurugu hakuna kizazi kitakachoendelea katika nchi yetu.
“Tumekutana leo hapa kwa ajili ya jukumu moja la kuiombea amani na upendo Taifa letu la Tanzania kuelekea uchaguzi. Tunatamani kuona Watanzania watakwenda kupiga kura zenye wingi wa amani na upendo.
“Tunaunga mkono jitihada za viongozi wetu kuthamini haki ya kila Mtanzania kikatiba kwamba baada ya miaka mitano lazima uchaguzi mkuu ufanyike.Hili siyo jambo la kufanyia propaganda za chuki, vurugu au vita.
“Ni suala la kulipokea kwa baraka kwa sababu hili ni jambo linaloandaa kizazi kwani tumeshuhudia katika nchi za majirani nyakati kama hizi za uchaguzi vizazi vingi vinapotea lakini sisi Watanzania tunawakuwa pamoja kwa ajili ya kufanya uchaguzi wenye amani na upendo kwa sababu Rastafali wanaishi kwa misingi ya amani na upendo.”
Pia amesema Tastafali hawako nyuma kuunga mkono kuhakikisha haki ya kimsingi ya kikatiba wanakwenda kuitekeleza katika hali iliyotulivu huku akifafanua kupitia imani yao ya Rastafali wanajisikia vibaya watu wakihamasisha vurugu.
“Ndio maana tukaona ipo haja kutokaa nyumbani, tumetoka barabarani kutembea kwenye jamii zote kuhamasisha amani na upendo ndiyo msingi wetu ambao unaoifanya Tanzania kuwa kitovu cha amani.
“Ikipotea amani katika nchi yetu hatuna pa kwenda hata biashara zinazofanyika watakosa wa kumuuzia. Amani na upendo tumeirithi kutoka waasisi wa taifa hili, tunafurahia maisha lakini tuna kizazi chetu kinachokuja ambacho kama hatujakiachia amani na upendo maana yake tumekiacha kife kipotee.
Mfalme Valelian Bagaile Kuwani Mkuu wa Imani ya Rastafali nchini amesisitiza hakuna sababu ya kuambatana na watu wanaochochea vita katika nchi yetu.”Mama Samia Suluhu Hassan kipaumbele chake kikuu ni amani na upendo kuhakikisha uchumi wa mtu mmoja mmoja unawafikia pale walipo.”
Aidha amesema Rastafali wanatamani kuona Dk.Samia Suluhu Hassan anarudi tena madarakani na ombi lao kubwa wanaomba imani ya Rastafali itambulike kama imani nyingine kwa sababu inaishi kwa kuenzi mila, desturi na jadi za mababu.
“Sisi imani yetu inaenzi ufalme, uchifu na tiba mbadala, hivyo tuendelee kushirikiana na jamii kwa amani na upendo.”







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...