Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

BARAZA la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Kwa kutambua nafasi ya vyombo vya habari katika kuelimisha jamii kuhusu masuala ya kiuchumi, limekutana na waandishi wa habari kwa lengo la kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu majukumu yake na namna linavyotekeleza shughuli za uwezeshaji nchini.

Akizungumza Mapema leo Oktoba 10, 2025, Kaimu Katibu Mtendaji wa NEEC, Bi. Neema Mwakatobe, amesema kupitia ushirikiano huo na waandishi wa habari, wananchi wataweza kupata uelewa mpana kuhusu kazi na majukumu ya Baraza hilo kupitia vipindi mbalimbali vitakavyorushwa kwenye vyombo vya habari.

Amesema ni muhimu kwa wananchi kufahamu kuwa wakipata changamoto waende wapi, fursa zilizopo za uwezeshaji na kwanini Baraza hili lipo ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kujikwamua kimaendeleo.

“Kupitia ninyi waandishi wa habari, jamii itapata nafasi ya kufahamu kwa undani namna Baraza linavyoratibu shughuli za uwezeshaji kiuchumi, pamoja na fursa zinazotolewa kwa Watanzania kushiriki katika uchumi wa nchi,” amesema Bi. Mwakatobe.

Ameeleza kuwa NEEC ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na jukumu lake kuu ni kufuatilia na kutathmini shughuli zote za uwezeshaji wananchi kiuchumi zinazotekelezwa nchini.

Ameongeza kuwa Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ilianzishwa mwaka 2004 na kufuatiwa na Sheria ya mwaka 2005 iliyoanzisha rasmi Baraza hilo kwa madhumuni ya kuratibu, kufuatilia na kuhakikisha wananchi wanashiriki ipasavyo katika shughuli za kiuchumi.

Bi. Mwakatobe amesema Baraza hufanya kazi kwa karibu na wizara, taasisi, na wadau mbalimbali wenye programu na bajeti za kuwawezesha wananchi, na hufuatilia utekelezaji wake ili kuhakikisha wananchi wanafikiwa kikamilifu.

Aidha, amesema ni wajibu wa NEEC kujua wadau wote wanaotekeleza shughuli za uwezeshaji na kutoa taarifa kwa umma kuhusu fursa zilizopo, ili wananchi wapate taarifa sahihi za uwezeshaji.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari (JOWUTA), Selemani Msuya, amesema chama hicho kinaishukuru NEEC kwa kutoa elimu hiyo muhimu kwa wanachama wao, jambo litakalosaidia kuongeza uelewa wa wanahabari kuhusu shughuli za Baraza hilo.

"Tunashukuru NEEC kwa kutambua mchango wa waandishi wa habari. Kupitia semina hii, wanachama wetu watakuwa mabalozi wazuri wa kufikisha taarifa za uwezeshaji kwa wananchi,” amesema Msuya.

Amesema hadi sasa JOWUTA ina wanachama zaidi ya 500 nchini, wakiwemo zaidi ya 150 kutoka mkoa wa Dar es Salaam, na ameiomba NEEC kuendelea kutoa mafunzo kama hayo kwa wanahabari wa mikoa mingine ili kuendelea kuelimisha umma kwa usahihi.

Katika semina hiyo, mada nne zimewasilishwa, ambazo ni:

1. Mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi

2. Ushiriki wa Watanzania katika uchumi

3. Utoaji wa huduma za biashara

4. Muongozo wa watoa huduma za biashara




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...