Na. OWM KVAU – Mbeya

Serikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaendelea kutekeleza mikakati kuhakikisha vijana wanapata fursa sawa za kujiletea maendeleo binafsi na kuchangia katika ustawi wa Taifa kwa ujumla.

Mikakati hiyo inajumuisha uanzishaji wa mifumo ya kitaasisi, kisera, mipango kazi, miongozo na sheria zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili vijana katika nyanja tofauti za kijamii na kiuchumi.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bi. Mary Maganga wakati wa Ufunguzi wa Kongamano la siku mbili la Vijana Tanzania linalofanyika kuanzia leo 12 Oktoba hadi 13 Oktoba, 2025 Jijini Mbeya katika Ukumbi wa City Park Garden.

Bi. Mary Maganga, amesema lengo la kongamano hilo ni kuwajengea vijana ujuzi na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, kukuza ushirikiano na ubadilishanaji wa mawazo, pamoja na kutambua na kuunga mkono mipango na miradi ya vijana inayolenga kuinua uchumi wao.

“Vijana ni nguvu ya mabadiliko na maendeleo katika jamii zetu. Ni lazima tutumie vema nguvu hii kubadilisha dunia kuwa mahali bora kwa ajili ya wote,” amesema Katibu Mkuu huyo.

Aidha, amewataka vijana kutumia kongamano hilo kama fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto zinazowakabili, ili Serikali iweze kuyachukua maoni yao na kuyatumia kuboresha sera, sheria, kanuni na miongozo kwa manufaa ya Vijana wote nchini.

Sambamba na hilo, Bi. Mary amewahimiza vijana kote nchini kujitokeza kushiriki katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, kwa kuchagua viongozi wanaoakisi matumaini, malengo na ndoto za taifa hili.

Awali Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya Rodrick Mpogolo aliwasihi vijana kuendelea kuipenda nchi na kujivunia Taifa la Tanzania kwa kuwa ni mahala ambapo kila kijana ana mchango wa kuleta maendeleo.

Akizungumza kuhusu idadi ya washiriki wa kongaamano hilo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Seleman Mvunye alisema limehusisha zaidi ya vijana 1,500 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na Maafisa Vijana toka Halmashauri zote nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...