Kwa sasa Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa miradi 13 ya dharura katika mkoa wa Lindi ambayo itatumia jumla ya shilingi Bilioni 119 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo ya dharura.

Miradi hiyo ni pamoja na Ujenzi wa Daraja la Kipwata (Mita 40) na Boksi kalavati eneo la Sakura na Songas, Ujenzi wa Daraja la Mikereng’ende (mita 40) na Boksi kalavati katika maeneo ya Mtandango/Stakshari na Masaninga, Ujenzi wa Boksi kalavati la Mbwemkuru I (seli 4, 5m x 4m), na matuta ya kuzuia mmomomnyoko wa udongo ( Spur dykes), Ujenzi wa Daraja la Somanga Mtama (60m) na Ujenzi wa Daraja la Njenga II (60m) ambapo miradi yote hii ipo katika barabara Kuu ya Marendego – Lindi – Mingoyo

Miradi mingine ni Ujenzi wa Daraja la Miguruwe (39m) pamoja na Boksi kalavati nne (4), Ujenzi wa Daraja la Zinga (18m) na Ujenzi wa Daraja la Kimambi (39m) ambayo ipo katika Barabara ya Mkoa ya Nangurukuru – Liwale.

Fedha hizo zinaendelea na utekelezaji wa miradi ya Barabara ya Mkoa ya Liwale – Nachingwea ambayo ni Ujenzi wa Daraja la Nangano (20m) na Makalavati ya Dharura ya mawili ya vipimo 2x2, mawili ya vipimo 5x2.5, Ujenzi wa Daraja la Mbwemkuru II (64m). Katika Barabara ya Mkoa ya Kiranjeranje- Namichiga serikali inaendelea na Ujenzi wa Daraja la Nakiu (70m) na Ujenzi wa Daraja la Kigombo (25m) na kalavati ya vipimo vya 5x4 huku katika Barabara ya Mkoa ya Tingi – Kipatimo Ujenzi wa Makalavati sita (6) ukiwa unaendelea.

Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua hatua zilizofikiwa za ujenzi wa miradi hiyo Msimamizi wa kitengo cha miradi ya Maendeleo TANROADS Mkoa wa Lindi Mhandisi Fred Sanga amesema kuwa mpaka sasa jumla ya shilingi Bilioni 58.5 zimeshalipwa kwa mkandarasi na kazi inaendelea kwa kasi ambayo itakamilika Disemba mwaka huu.

Aidha, Mhandisi Sanga amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 serikali imepanga kutumia Bilioni 16.2 kwa ajili ya Miradi ya Matengezo (Maintenance) kwa gharama ya Shilingi bilioni 13.3 huku Miradi ya Maendeleo (Development) ikitarajiwa kutumia shilingi Bilioni 2.9 kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 405.15 za barabara za lami sambamba na ujenzi wa kilomita 901.54 za barabara za Changarawe.

Mhandisi Sanga amesema kuwa katika mpango huo kutakuwa na ujenzi wa madaraja 3 katika barabara ya Kilwa Masoko – Liwale, barabara ya Matangini -Chiola - Likunja na barabara ya Chiola – Ruponda

Kuanzia Oktoba, 2023 hadi kufikia Mei, 2024 Tanzania ilikumbwa na kadhia ya mvua kubwa zilizotawala zikichangiwa na tukio la asili la hali ya hewa El-Nino pamoja na Kimbunga Hidaya lililoathiri hali ya hewa nchini na kusababisha athari hasi kwa wananchi kukosa makazi, vifo, magonjwa ya milipuko, uharibifu wa miundombinu ya barabara pamoja na madaraja.

Katika eneo la Miundombinu, Barabara za Mkoa wa Lindi ziliathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na madhara ya mvua hizo zilizonyesha mfululizo ambapo hata hivyo Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan ikatoa fedha jumla ya Shilingi za kitanzania bilioni 19 kwa ajili ya matengenezo ya dharula na kurejesha mawasiliano kwa haraka.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...