Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Elisius Mhelela, amesema kuwa kila siku ni siku ya kuhudumia wateja, akiweka wazi kuwa maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja ni fursa muhimu ya kutambua mchango mkubwa wa wateja kwa shirika hilo.
Ameyasema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki hiyo yaliyofanyika katika ofisi za TANESCO mkoa wa Ruvuma, chini ya kaulimbiu isemayo “Mpango Umewezekana.”
Akizungumza mbele ya wafanyakazi wa TANESCO pamoja na wadau wengine waliohudhuria hafla hiyo, Mhandisi Mhelela alihimiza mshikamano na ushirikiano miongoni mwa watumishi wa shirika hilo ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa na matokeo chanya kwa wananchi.
Alisema kuwa mafanikio yanapatikana kwa juhudi za pamoja na si kwa maneno tu, akisisitiza kuwa hata changamoto zinapojitokeza ni vyema kushughulikiwa kwa umoja.
Mhandisi Mhelela alieleza kuwa jukumu la msingi la TANESCO ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, kwani huduma hiyo ni kichocheo kikuu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Alibainisha kuwa maelekezo ya serikali ni kuhakikisha umeme unawafikia wananchi wote bila ubaguzi na shirika hilo limejipanga kuhakikisha hilo linawezekana.
Akizungumzia hali ya usambazaji wa umeme katika mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Mhelela alisema kuwa zaidi ya vijiji 550 tayari vimeshapatiwa huduma ya umeme, alifafanua kuwa mkoa huo una jumla ya vitongoji 3,691 na kati ya hivyo, ni asilimia 53 tu ya vitongoji ambavyo tayari vimeunganishwa na umeme, amesema juhudi zinaendelea ili kuhakikisha vitongoji vilivyosalia navyo vinapata huduma hiyo muhimu.
Aliongeza kuwa wananchi wengi wa mkoa wa Ruvuma wana hamu kubwa ya kupata umeme, hivyo TANESCO inatakiwa kuongeza kasi na kuboresha utendaji ili kuendana na matarajio ya wananchi, alikiri kuwa bado kuna kazi kubwa mbele yao, lakini kwa mshikamano shirika hilo litaweza kufanikisha malengo ya kuwafikishia wananchi nishati ya umeme kwa wigo mpana zaidi.
Katika hitimisho lake, Mhandisi Mhelela alisisitiza dhamira ya TANESCO ya kuendelea kuwahudumia Watanzania kwa uaminifu na kujituma, huku akiwataka wafanyakazi wa shirika hilo kuendelea kutoa huduma kwa weledi, ili kuongeza imani ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia nishati ya umeme.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...