Maombi Maalum ya Wanawake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu yamefanyika leo Oktoba 26 katika Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma, yakilenga kuliombea Taifa liweze kufanikisha uchaguzi wa amani, utulivu na maendeleo.
Maombi hayo yamehudhuriwa na waumini wanawake na viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali yakiwemo BAKWATA, TEC, CCT, CPCT, KKKT, Mashahidi wa Yehova, na Wasabato, ambao kwa pamoja wameomba Mungu alijalie Taifa uchaguzi salama na wenye kumpa ushindi kiongozi mwenye maono ya maendeleo kwa Watanzania.
Akizungumza katika maombi hayo mgeni rasmi Waziri wa Afya Jenista Mhagama, amewataka wanawake wa Mkoa wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kuwachagua viongozi wenye sera bora zitakazoboresha huduma muhimu kama afya, kilimo, na uchumi.
Mhagama amesema maombi hayo ni muhimu kwa wanawake kwani yana nafasi ya kipekee katika kumuomba Mungu awape hekima na macho ya kuona viongozi wenye nia njema ya kutumikia wananchi, ameongeza kuwa wanawake wanapaswa kuwa mabalozi wa amani kutokana na ushawishi wao mkubwa katika jamii.
“Ni jukumu letu kuhakikisha amani inatawala katika Mkoa wa Ruvuma na nchi yetu kwa ujumla. Tusikubali kugawanyika kwa misingi ya dini, kabila au itikadi za kisiasa."
Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleza misingi ya amani na utulivu nchini, huku serikali anayoiongoza ikiendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi inayolenga kuinua uchumi wao na kusogeza karibu huduma za kijamii kwa wananchi.
Mhagama pia amewahimiza wananchi wote waliofikisha umri wa miaka 18 kuhakikisha wanatumia haki yao ya kikatiba kwa kujitokeza kupiga kura tarehe 29 Oktoba mwaka huu, ili kuchagua viongozi watakaoliletea Taifa maendeleo chanya.
Maombi hayo yamehitimishwa kwa sala za pamoja za kuombea uchaguzi, viongozi wa nchi na ustawi wa Taifa la Tanzania.


.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...