Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema ukarabati wa reli ya TAZARA utaimarisha Ukanda wa Kati na Kusini, kuchochea biashara Tanzania, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Bara la Afrika kwa ujumla.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la uzinduzi wa Ukarabati Mkubwa wa Reli ya TAZARA iliyofanyika Jijini Lusaka nchini Zambia.
Ameongeza kwamba ukarabati huo, utaongeza mauzo ya bidhaa nje na ndani ya Mataifa ya Zambia na Tanzania, kukuza kilimo, madini, viwanda, utalii na kutengeza ajira zaidi kwa wananchi wa ukanda huo.
Makamu wa Rais amesema wakati reli ya TAZARA inaimarishwa, Tanzania inafanya maboresho ya kisasa ya bandari ikiwemo dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam kwa magati mapya, kuboresha ufanisi, na kuhakikisha muunganiko mzuri wa Reli ya Umeme ya Kisasa (SGR) na TAZARA. Ameongeza kwamba, Tanzania itaendelea kuboresha bandari za Tanga, Mtwara na Bagamoyo ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na ubora wa kimataifa wa usafirishaji kwa nchi za Zambia, SADC na Afrika kwa ujumla.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema ukarabati huo unakuja wakati China inaibuka kama mdau muhimu wa ukuaji wa uchumi kimataifa chini ya mpango wake wa 15 wa Miaka Mitano. Amesema hali hiyo inaiweka China kama mshirika muhimu wa maendeleo.
Makamu wa Rais amesema historia inafundisha ukweli wenye nguvu kwamba, Tanzania, Zambia na China zinaposimama pamoja, hakuna changamoto iliyo kubwa sana. Amesema ikiwa waasisi wa mataifa hayo, waliweza kujenga Reli ya Uhuru, kwa sasa ikizingatiwa mataifa na uwezo yaliyonayo yataweza kukarabati Reli ya TAZARA na kuifanya kuwa mfano wa ushirikiano wa karne ya 21.
Mamlaka ya Reli ya Tanzania–Zambia (TAZARA) ni mojawapo ya alama muhimu za urafiki, ushirikiano, na matarajio ya pamoja kati ya Serikali za Tanzania, Zambia na Jamhuri ya Watu wa China. Reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,860 ikiwa na kilomita 975 kwa Tanzania na kilomita 885 nchini Zambia reli hiyo inaunganisha Bandari ya Dar es Salaam na Kapiri-Mposhi Mpya, kwa kutumia mfumo wa Cape Gauge (milimita 1,067).
Uwekezaji katika ukarabati huo utafanya uboreshaji mkubwa, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa njia ya reli, stesheni, mifumo ya mawasiliano, pamoja na ununuzi wa treni 34, mabehewa 760, makochi 18 na treni 2 kwa ajili ya huduma za abiria. Ufufuaji huo unalenga kuongeza usafirishaji wa mizigo hadi kufikia tani milioni 2.4 ifikapo mwaka wa tatu wa uendeshaji.
Ukarabati mkubwa wa Reli ya TAZARA ni hatua muhimu katika historia ya miundombinu ya Reli ya Tanzania-Zambia. Ukarabati huo ni fursa, ukiweka reli kama njia muhimu ya kikanda ambayo itachochea uwekezaji na biashara pamoja na kupunguza gharama za usafirishaji na kukuza ushirikiano wa kikanda. Zaidi ya hayo, mradi huo ni msingi katika kuimarisha uhusiano kati ya China na Tanzania na Zambia, huku ukiimarisha uhusiano kati ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Hafla hiyo imehudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Hakainde Hichilema pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Li Qiang.
Katika hafla hiyo, Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Nchimbi ameambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara, Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Balozi Luteni Jenerali Mathew Mkingule, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Mhandisi Machibya Masanja, Mkurugenzi Mkuu TASAC Bw. Mohamed Salum pamoja na Wataalamu mbalimbali kutoka Serikalini.










Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...