Na. Benny Mwaipaja, Accra, Ghana
Rais wa Ghana, Mhe. John Dramani Mahama, amewataka Wahasibu Barani Afrika kuhakikisha kuwa wanazishauri na kuzisimamia nchi zao kuwa na matumizi sahihi ya fedha za umma ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi hizo kwa kutumia mifumo thabiti ya kidigitali na akili unde (artificial Intelligence).
Mhe. Mahama ametoa wito huo Mjini Accra nchini Ghana, wakati akifungua Mkutano wa Tatu wa Jumuiya ya Wahasibu wa Serikali barani Afrika (African Association of Accountants General Meeting (AAAG), unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Accra (AICC), unaolenga kujadili namna kada hiyo ya wahasibu inavyoweza kuchangia maendeleo ya nchi zao kwa kuhakikisha kuwa kunakuwa na uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma na rasilimali nyingine.
Alisema kuwa Afrika imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi, yakiwemo madini, gesi ardhi na rasilimali nyingine, lakini Bara hilo limeendelea kuwa katika hali ya umasikini kutokana na kukosekana kwa uwajibikaji na uadilifu wa matumizi ya rasilimali hizo hali inayokwaza maendeleo ya wananchi.
Alitolea mfano wa sekta ya ununuzi ambayo alisema kuwa imekuwa ikitumika kupoteza fedha nyingi za Serikali kutokana na gharama kubwa za kandarasi za utekelezaji wa miradi ya Serikali ambazo haziendani na hali halisi ya bei katika soko.
Alitoa rai kwa Wahasibu wa Serikali katika nchi za Afrika kuwa jicho la umma kwa kuhakikisha kuwa wanaweka na kutumia mifumo thabiti ya kuzuia upotevu wa fedha na kuwashauri watawala kujali maslahi ya wananchi.
Kwa upande wake, Mhasibu Mkuu wa Serikali ya Tanzania, CPA Leonard Mkude, alisema kuwa mkutano huo utaweka maazimio ya namna ya kuongeza uwazi na uwajibikaji wa matumizi ya fedha za umma yatakayowasilishwa kwa Wakuu wa Nchi za Afrika kwa ajili ya kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazotokana na matumizi ya fedha za umma.
Alisema kuwa Kada ya Wahasibu ni Kada muhimu inayotakiwa kuweka misingi mizuri ya matumizi sahihi ya fedha za umma kwa kuwa ndiyo inayohusika na malipo ya kila siku ya huduma na utekelezaji wa miradi ya wananchi inayofanywa na Serikali.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wahasibu wa Serikali Barani Afrika, Bw. Fredrick Riaga, alisema kuwa Mkutano huo uliobeba Kaulimbiu isemayo “Afrika ya Kesho: Kuimarisha Usimamizi wa Fedha za Umma kwa ajili ya Ustawi wa Kiuchumi", umewahusisha washiriki zaidi ya 2,000 kutoka nchi 55 za Afrika, umelenga kuweka mikakati ya pamoja ya namna ya kusimamia matumizi sahihi ya fedha za umma.
Mkutano huo ambao pia ulizikutanisha Jumuiya za wafanyabiashara na wadau wengine, umehudhuriwa na viongozi wengine mashuhuri akiwemo Mwanzilishi wa Mfuko wa P.L.O Lumumba, Profesa Patrick Loch Otieno Lumumba, mabaye alikuwa miongoni wa watoa mada walioalikwa.
Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA. Leonard Mkude, akifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Ghana, Mhe. John Dramani Mahama (hayupo pichani), wakati akifungua Mkutano wa Tatu wa Jumuiya ya Wahasibu wa Serikali barani Afrika, wenye kaulimbiu ya Afrika ya Kesho: Kuimarisha Usimamizi wa Fedha za Umma kwa ajili ya ustawi wa kiuchumi, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Accra (AICC), nchini Ghana. ambapo pamoja na mambo mengine alisema kuwa nchi za Afrika zinapaswa kujiendeleza kwa kutegemea rasiliamali zake ili kukuza uchumi kwa haraka.
Baadhi ya ujumbe wa Tanzania ambao ni wahasibu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi mbalimbali za Tanzania wakifuatilia mada kuhusu Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM) kama kichocheo cha ukuaji endelevu, iliyokuwa inatolewa na Mkurugenzi wa Hesabu za Taifa, Ghana, Dkt. Mc-Effort Adadey, wakati wa Mkutano wa Tatu wa Jumuiya ya Wahasibu wa Serikali barani Afrika wenye kaulimbiu ya Afrika ya Kesho: Kuimarisha Usimamizi wa Fedha za Umma kwa ajili ya ustawi wa kiuchumi, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Accra (AICC), nchini Ghana

Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA. Leonard Mkude (Katikati), akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Wizara ya Fedha na Taasisi zingine za Serikali baada ya kuhudhuria ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Jumuiya ya Wahasibu wa Serikali barani Afrika, wenye kaulimbiu ya Afrika ya Kesho: Kuimarisha Usimamizi wa Fedha za Umma kwa ajili ya ustawi wa kiuchumi, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Accra (AICC), nchini Ghana.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...