CHAMA cha Mawakili wa Serikali kinatoa Pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Hamza Saidi Johari kwa kuaminiwa na kuteuliwa kwa Mara ya pili mfululizo kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa Sifa na Ubobevu alionao ni dhahiri anazo Sifa za kumfanya kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwani tukirejea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 59 inabainisha wazi kuhusu nafasi na sifa za Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama ifuatavyo:
Ibara ya 59.- (1)
Kutakuwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambaye katika ibara zifuatazo za Katiba hii atatajwa tu kwa kifupi kama “Mwanasheria Mkuu” ambaye atateuliwa na Rais.
(2) Mwanasheria Mkuu atateuliwa kutoka miongoni mwa watumishi wa umma wenye sifa ya kufanya kazi za uwakili au watu wenye sifa ya kusajiliwa kuwa wakili, na ambaye amekuwa na sifa hizo mfululizo kwa muda usiopungua miaka kumi na tano.
Kwa mujibu wa kipengele hicho cha Katiba, ni wazi kwamba uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali si wa kisiasa bali unatokana na uzoefu na sifa za kitaaluma. Hivyo basi, ni muhimu kwa kila mmoja wetu kutambua kuwa viongozi wa umma, hasa wale wanaoteuliwa kwa mujibu wa Katiba, hupitia taratibu za kisheria na kiutendaji kabla ya kuteuliwa.
Taarifa zozote zinazotolewa zisiso sahihi kuhusu viongozi hawa ni kitendo kinachoweza kuathiri heshima ya taasisi za umma na kupotosha jamii.
Ni wajibu wa kila Mtanzania kutafuta taarifa sahihi kutoka katika vyanzo rasmi kama vile Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au tovuti rasmi za serikali kabla ya kueneza au kuamini taarifa mtandaoni.
Aidha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Saidi Johari ana uzoefu mkubwa na wa muda mrefu kwa zaidi ya miaka 20 kama mtumishi wa umma Mwandamizi aliyebobea katika eneo la majadiliano ya mikataba, Sheria za anga, Sheria ya Bahari na Sheria za udhibiti.
Zaidi ya hayo anazo Sifa stahiki za Kitaaluma, ikiwemo Shahada ya Kwanza ya Sheria (LL. B) na Shahada ya Uzamili ya Sheria (LL.M) katika Sheria ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Kiev katika Jamhuri ya Ukraine na ana cheti cha Uongozi na Usimamizi kutoka Chuo cha Wafanyakazi wa Utawala cha India. Amehudhuria mafunzo mbalimbali ya kitaaluma na kuchapisha maandiko na vitini kadhaa katika
majadiliano ya Mikataba, Sheria ya Usafiri wa Anga na Sheria ya Bahari.
Vilevile amekuwa Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la Huduma za Anga (CANSO) kwa Kanda ya Afrika na mjumbe wa Kamati Tendaji ya CANSO kwa miaka sita na Mwenyekiti wa Kamati ya Kisheria ya CANSO. Amewahi pia kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usafiri wa Anga ya SADC na Mwenyekiti wa Wakala wa Usalama wa Usafiri wa Anga wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (CASSOA).
Aidha, Mhe Hamza Johari ambaye ni mlezi wa Chama Cha Mawakili wa Serikali na ni Wakili namba moja kwa mujibu wa Sheria na ni Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mwenyekiti wa Jopo la Ithibati ya Wasuluhishi, Wadadisi, Wasuluhishi na Waamuzi, Mwenyekiti wa Timu ya Wanasheria wa Serikali, Mjumbe wa Kamati ya Taifa ya Uendeshaji Uwekezaji na Mjumbe wa Kamati ya Mawakili (the Advocates Committee) . Pia aliwahi kuwa Mwanachama Mfadhili wa Taasisi ya Kimataifa ya Usafirishaji (CILT) iliyoanzishwa na Royal Charter 1929 (Uingereza), Mwanachama wa Maisha (lifetime), Chuo cha Wafanyakazi wa Utawala cha India na mwanachama wa Taasisi ya Wakurugenzi nchini Tanzania.
Mhe. Hamza Saidi Johari amefanya kazi kama Mkurugenzi Mkuu katika Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania kwa miaka tisa akitekeleza Sheria ya Usafiri wa Anga, Sura ya 80 ya Sheria. Amekuwa Mhadhiri mgeni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Mzumbe na Chuo Kikuu cha Alexandria (Misri) katika Sheria za Kimataifa za Bahari na Sheria za Kimataifa za Usafirishaji (Ardhi, Anga na Bahari).
Ameshiriki katika majadiliano ya miradi kadhaa ya Serikali kuhusu bandari za baharini, usafiri wa anga na migogoro ya kimataifa ya bweni kama Mwenyekiti wa Timu za Majadiliano za Serikali (GNT) na Mjumbe wa Kikosi Kazi mbalimbali cha Kitaifa na Kamati za Uongozi kama ifuatavyo:
1. Mjumbe wa Timu ya Kikosi Kazi cha Taifa kuhusu mgogoro wa Mpaka kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi;
2. Mjumbe wa Timu ya Kikosi Kazi cha Taifa kuhusu mgogoro wa Mpaka kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Burundi;
3. Mjumbe wa Timu ya Kikosi Kazi cha Taifa kuhusu mgogoro wa Mpaka kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Uganda;
4. Kushirikishwa kama mtaalam wa maoni ya kisheria na Serikali ya Japani juu ya mzozo kati ya Japan na Uchina kuhusu Kisiwa cha Senkaku;
5. Mpatanishi Kiongozi wa Timu ya Serikali kuhusu Mikataba ya Huduma za Ndege baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Marekani, Canada, Uingereza, Ufaransa, Italia, Hispania, China, Russia, Falme za Kiarabu, Ujerumani, Uholanzi, Afrika Kusini, Oman, Korea Kusini, Morocco na Kenya;
6. Mwenyekiti wa Timu ya Majadiliano ya Serikali kuhusu marekebisho ya Mkataba wa Makubaliano kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania na Huduma za Makontena ya Kimataifa (TICTS);
7. Mwenyekiti wa Timu ya Majadiliano ya Serikali kuhusu marekebisho ya Mkataba wa Wanahisa na Miamala mingine ya Kibiashara kati ya Serikali na PUMA Energy;
8. Mwenyekiti wa Timu ya Majadiliano ya Serikali kuhusu marekebisho ya Makubaliano ya Wanahisa kati ya Serikali na TIPPER;
9. Mwenyekiti wa Timu ya Majadiliano ya Serikali kuhusu marekebisho ya Mkataba wa wenye Hisa kati ya Serikali na Progress Rail ya Marekani kwa ajili ya ununuzi wa Locomotives kwa Shirika la Reli Tanzania;
10. Mwenyekiti wa Timu ya Majadiliano ya Serikali kuhusu kusitisha Mkataba wa Makubaliano kati ya Mamlaka ya Bandari Tanzania na Huduma za Kimataifa za Makontena Tanzania (TICTS);
11. Mpatanishi Kiongozi wa Timu ya Majadiliano ya Serikali ya Ubia na kuendeleza Makubaliano ya Kiserikali (IGA) kwa ajili ya kuendeleza Bandari ya Dar es Salaam kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Emirate ya Dubai;
12. Mpatanishi Kiongozi wa Timu ya Majadiliano ya Serikali kwa ajili ya majadiliano ya Mkataba wa Serikali Mwenyeji (HGA) kati ya Serikali na DP World ya U.A.E;
13. Mpatanishi Kiongozi wa Timu ya Majadiliano ya Serikali kwa ajili ya majadiliano ya Mkataba wa Makubaliano kati ya Serikali na DP World ya U.A.E;
14. Mpatanishi Kiongozi wa Timu ya Majadiliano ya Serikali kwa ajili ya Mkataba wa Ukodishaji kati ya Serikali na DP World ya U.A.E kwa ajili ya kukodisha ardhi katika Bandari ya Dar es Salaam;
15. Mpatanishi Kiongozi wa Timu ya Majadiliano ya Serikali kwa ajili ya majadiliano ya Mkataba wa Makubaliano kati ya Serikali na Bandari ya Adani ya India kwa ajili ya huduma za makontena katika Bandari ya Dar es Salaam;
16. Mpatanishi Kiongozi wa Timu ya Majadiliano ya Serikali ya majadiliano ya Mkataba wa Ukodishaji kati ya Serikali na Bandari ya Adani ya India kwa ajili ya ukodishaji wa ardhi katika Bandari ya Dar es Salaam.
Huyo ndiye Hamza Saidi Johari Wakili namba moja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mmakonde mzaliwa wa wilaya ya Mtwara Vijijini, Tarafa ya Ziwani kata ya Nalingu.
Imetolewa na CHAMA CHA MAWAKILI WA SERIKALI TANZANIA


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...