Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Wanadiplomasia wanaowakilisha nchi na taasisi za kimataifa hapa nchini katika Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo, ambao ni wa kwanza tangu kuundwa kwa Serikali ya Awamu ya Sita kipindi cha pili baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, ulilenga kuimarisha majadiliano na kueleza msimamo wa Serikali kuhusu masuala ya kitaifa na kimataifa.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Waziri Kombo aliwahakikishia wanadiplomasia hao kuwa Tanzania itaendelea kudumisha na kuimarisha ushirikiano na mataifa yote pamoja na mashirika wanayoyawakilisha.
Kupitia kikao hicho, Mabalozi kutoka nchi mbalimbali wamethibitisha utayari wa nchi na tasisi zao kuendelea kushirikiana na Tanzania, hatua ambayo Waziri Kombo alisema kuwa inaonesha ukomavu wa diplomasia na uhusiano imara baina ya Tanzania na washirika wake wa kimataifa.
Serikali pia ilitumia mkutano huo kutoa taarifa kwa wanadiplomasia kuhusu mwenendo wa uchaguzi mkuu na matukio wakati wa uchaguzi huo na kuelezea hatua zilizochukuliwa na Serikali kurejesha hali ya utulivu, kuhakikisha usalama wa raia na mali zao, na kuendeleza utoaji wa huduma za msingi na shughuli za kiuchumi.
Mhe. Waziri Kombo pia aliwaeleza mabalozi hao juu ya Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchunguza chanzo cha matukio hayo, pamoja na kupendekeza hatua madhubuti za kuimarisha mifumo ya kitaifa ili kuzuia matukio kama hayo kutokea tena.





















Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...