NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limehimiza wananchi kuzingatia matumizi ya chakula salama pamoja na kuimarisha usafi katika maandalizi ya chakula ili kulinda afya ya mlaji na kupunguza madhara yanayotokana na vyakula visivyo salama.

Akizungumza leo Novemba 21, 2025 Jijini Dar es Salaam, Afisa Udhibiti Ubora Mkuu wa TBS, Bw. Moses Mbambe, amesema usalama wa chakula unategemea kwa kiasi kikubwa maandalizi yanayozingatia usafi na matumizi ya maji salama.

“Chakula salama ni kile kilichoandaliwa katika mazingira safi, kisichokuwa na bakteria au vimelea vinavyoweza kusababisha maradhi kwa mlaji,” amesema Mbambe.

Mbambe amesema matumizi ya maji machafu katika maandalizi ya chakula, pamoja na kupikia katika mazingira yasiyo safi au vyenye maandalizi hafifu, huathiri kwa kiasi kikubwa usalama wa chakula kinachotumika majumbani, kwenye migahawa na katika maeneo ya biashara.

Katika kuongeza usalama wa chakula, TBS imehimiza uhifadhi sahihi wa vyakula hususan nafaka kwa kuzihifadhi kwenye madumu yenye mfuniko ili kuzuia mashambulizi ya sumukuvu, ambayo yana madhara makubwa kiafya.

Vilevile, Mbambe amesisitiza umuhimu wa kutenganisha chakula kilichopikwa na kisichopikwa, pamoja na kupika vyakula kama nyama kwa muda sahihi ili kuua vimelea vya magonjwa.

TBS imeonya pia juu ya matumizi ya vyombo visivyo safi na usambazaji wa chakula kwenye vifungashio visivyo salama ikiwemo chupa zilizotumika awali kuhifadhia juisi, mafuta au bidhaa nyingine.

“Chakula kinapobaki lazima kipashwe angalau nyuzi joto 60°C ili kuua vimelea vinavyoweza kuleta athari kwa afya ya binadamu,” amesema Mbambe.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Tathmini ya Hatari za Chakula TBS, Bi. Immaculatha Justine, amesema vyakula vinavyotokana na mifugo ni muhimu kwa afya ya binadamu lakini vinaweza kuwa hatarishi endapo kanuni bora hazitazingatiwa kuanzia ufugaji, uchinjaji hadi usambazaji.

Ametaja vihatarishi vya kibailojia kama vile virusi vya homa ya manjano, bonde la ufa na minyoo kuwa miongoni mwa vimelea vinavyoweza kusababisha madhara ya kudumu kwa walaji.

Ameongeza kuwa matumizi holela ya dawa za mifugo bila kufuata ushauri wa wataalamu yanaweza kusababisha mabaki ya kemikali hatarishi kubaki katika mazao ya wanyama.

Kwa upande wa samaki wanaofugwa, Bi. Immaculatha ameainisha uwezekano wa kuwepo kwa mabaki ya madini tembo, ambayo husababisha athari za kiafya endapo yataliwa bila kudhibitiwa.

Bi. Immaculatha amehimiza kufuatwa kwa kanuni za usafi katika hatua zote za mnyororo wa thamani wa chakula cha mifugo, na amewataka wananchi kununua bidhaa za mifugo katika maeneo yaliyoidhinishwa na kukaguliwa na mamlaka husika.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...