Na Karama Kenyunko, michuzi TV
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda amewataka vijana kuwa mabalozi wa amani na uzalendo kwa taifa kwa kufuata sheria za kodi, akibainisha kuwa hakuna maendeleo ya biashara na ajira bila utulivu wa nchi.
Akizungumza katika mahafali ya 18 ya Chuo cha Kodi (ITA), Mwenda alisema vijana ndio kundi kubwa katika taifa na ndio waliobeba uchumi wa Tanzania kupitia ujasiriamali, ajira na kulipa kodi kwa uaminifu.
“Hakikisheni mnakuwa mabalozi wazuri katika kulinda na kusimamia amani,hakuna biashara, kuajiriwa wala kutimiza ndoto zenu kama hatuna amani na utulivu lakini kama kuna changamoto zinazotakiwa kutatuliwa tutafute njia nzuri ya kuzitatua,"alisema Mwenda.
Aliongeza,"vijana tuwe na uzalendo kwenye Taifa letu kwa kufuata Sheria za kulipa kodi lakini pia tuishi pamoja bila kujali dini wala kabila kwasababu sisi sote ni watanzania,"
Akizungumzia mkakati wa serikali kuhusu kutumia rasilimali za ndani, Mwenda alisema TRA haitegemei kuongeza viwango vya kodi kuimarisha uchumi, bali itapanua wigo wa walipa kodi kwa kutumia mifumo rafiki ya kidijiti pamoja na elimu kwa umma.
“Kujitegemea kwa mapato ya ndani haimaanishi kuongeza mizigo kwa walipa kodi bali ni kuongeza wigo wa kodi na kuwahudumia walipa kodi kwa haki,” alieleza na kuongeza kuwa "mamlaka itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara ambao biashara zao zimepata changamoto ili ziweze kurudi kama kawaida
Aidha alisema kuwa uwekezaji wa serikali kwenye mifumo ya kidijiti umeongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kuipongeza ITA kwa kuanzisha 'programu ya distance learning' itakayowezesha Watanzania wengi kupata elimu ya kodi, na kupunguza upotevu wa mapato ya serikali.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elija Mwandubya alisema serikali itaendelea kuwekeza katika Chuo hicho ili kiwe nguzo ya wataalamu, tafiti na ubunifu wa sera za kodi zinazochochea ukuaji wa uchumi.
Aidha,Alikitaka chuo hicho kuendelea kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kisasa, ikiwemo matumizi ya teknolojia za ukusanyaji kodi, usalama wa taarifa na forodha.
"Niwapongeze wahitimu wote 561 wa ngazi za vyeti, stashahada, shahada na uzamili, katumieni ujuzi mlioupata kujiendeleza na kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia ajira na ujasiriamali.Natambua kuwa sekta binafsi ina nafasi kubwa ya kukuza uchumi na kutoa ajira tumieni fursa zilizopo, msisubiri kuajiriwa serikalini pekee,” alisema.
Mwandubya aliwataka wadau mbalimbali, pamoja na taasisi za umma, kuwaunga mkono vijana wanaojiajiri, huku akiitaka serikali kuendelea kuondoa vikwazo vinavyokwamisha biashara.
“Tusiweke taratibu zinazozuia ukuaji wa biashara, tuwape nafasi vijana wetu waoneshe uwezo wao,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine,aliipongeza TRA kwa kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato, akibainisha kuwa kwa sasa mamlaka hiyo inavuka malengo ya makusanyo kwa zaidi ya asilimia 100 kila mwezi, rekodi ambayo haijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo.
Alisema hatua hiyo inaonyesha uadilifu na weledi wa watumishi wa TRA katika kusimamia rasilimali za nchi, na mchango wake mkubwa katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo
Mwandubya alisisitiza kuwa mafanikio hayo hayahusiani na ongezeko la viwango vya kodi, bali yanatokana na kupanua wigo wa walipa kodi na kuboresha mazingira ya biashara. “Nafasi ya kuongeza mapato si kuongeza kodi. Ni kuwashirikisha wengi uchumi unaokua na kulinda amani, kwani amani ni uchumi,”alisema.
Naye, Mkuu wa Chuo hicho,Profesa Isaya Jairo alisema wamefanikiwa kutoa mafunzo ya lazima kwa wafanyakazi 2673 lengo likiwa ni kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
"Tunajivunia kuongeza umahiri wa wataalamu wa kodi ili waendane na mabadiliko ya dunia. Mafunzo haya yamelenga kuimarisha utendaji katika ukusanyaji wa mapato ya serikali,” alisema Profesa Jairo.
Aliipongeza serikali kwa kuongeza wafanyakazi hadi kufikia asilimia 40 ya wafanyakazi wote kwa mwaka huu.




.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...