BANJUL, GAMBIA – Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, ametajwa kama moja ya nguzo muhimu katika mageuzi ya usimamizi wa misitu na wanyamapori barani Afrika, baada ya kutambuliwa rasmi kwa uongozi wake aliyouonyesha kama Mwenyekiti wa Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori Afrika (AFWC) anayemaliza muda wake.
Kutambuliwa huko kulitolewa katika Kikao cha 25 cha Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori Afrika (AFWC25) na Wiki ya 9 ya Misitu na Wanyamapori Afrika (AFWW9) kilichofanyika Desemba 1–5, 2025, jijini Banjul, Gambia, na kuhudhuriwa na zaidi ya wajumbe 200 kutoka mataifa yote ya Afrika. Profesa Silayo alisifiwa kwa “kuongoza bara katika kipindi cha mageuzi na kuweka msingi imara wa ushirikiano wa kikanda unaoimarisha mustakabali wa rasilimali za misitu na wanyamapori.”
Katika kufunga mkutano huo, Waziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Rasilimali Asilia wa Gambia, Hon. Rohey Manjang, alisema maamuzi na maazimio yaliyofikiwa ni hatua muhimu katika kuleta mwelekeo mpya wa bara katika uhifadhi. Alisema Serikali ya Gambia tayari imeongeza bajeti ya mwaka 2026 kwa ajili ya uhifadhi, urejeshwaji wa misitu na uimarishaji wa maeneo tengefu.
“Kazi haijaisha hapa; ndiyo kwanza imeanza. Afrika lazima ichukue hatua sasa na kuimiliki ajenda ya uhifadhi kama bara moja,” alisema Manjang.
Katika mjadala wa siku tano, wajumbe walichambua masuala ya uvumbuzi kwenye ufuatiliaji wa misitu, mifumo shirikishi ya usimamizi inayojumuisha jamii, wanawake na vijana, upatikanaji wa fedha za kijani na nafasi ya misitu kwenye uchumi wa jamii na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Katibu wa AFWC, Edward Kilawe, aliwataka wanachama kutekeleza maazimio ya Banjul, akisisitiza kuwa enzi ya kufanya kazi kwa kutengana imekwisha.
“Afrika ina uwezo na rasilimali za kutosha kulinda misitu na wanyamapori kupitia ubunifu na ushirikiano wa karibu,” alisema.
Alitaja uvunaji endelevu wa asali, ulinzi wa mikoko, na urejeshaji wa ardhi iliyoharibika kama mifano ya mbinu za kitaifa zinazoweza kuigwa barani kote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa AFWC, Ebrima Jawara, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mazingira ya Gambia, aliahidi kuwa ajenda za miaka miwili ijayo zitajikita kwenye uvumbuzi, ushirikishwaji wa wananchi na uimarishaji wa sera.
“Ubunifu si hiari tena, ni lazima. Na hauwezi kusonga bila ushirikiano wa wananchi,” alisema.
Katika risala ya shukrani, wajumbe walipongeza FAO na Serikali ya Gambia kwa maandalizi mazuri, huduma za wakalimani na ziara za mafunzo katika misitu ya mikoko, maeneo ya tiba asili na miradi ya ufugaji nyuki ambayo imeonesha mafanikio ya uhifadhi shirikishi.
Waziri Manjang alifunga mkutano kwa kuwatakia wajumbe safari njema na kuhimiza utekelezaji wa maamuzi: “Afrika ni moja. Utekelezaji wa maazimio haya ndiyo utakaothibitisha umoja huo.”







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...