MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, amewapongeza Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) kwa kuratibu na kushiriki kikamilifu mbio za marathon zilizolenga kuhamasisha juhudi za kuboresha miundombinu ya elimu katika chuo hicho.

Akizungumza leo Desemba 6, 2025, mjini Bagamoyo mkoani Pwani, Mhe. Ndemanga alisema ni muhimu kwa taasisi kama ADEM kutambua nafasi ya mazoezi ya mwili kwa watumishi wake kwani yanasaidia kuwaweka sawa kiakili na kimwili, jambo linaloongeza ufanisi katika utendaji wao wa kazi.

“Niwapongeze ADEM kwa maandalizi mazuri ya mbio hizi ambazo zimekuwa za mfano kutokana na kuwa na washiriki wengi kutoka ndani ya taasisi,” amesema.

Aidha, DC Ndemanga amewashauri washiriki wa ADEM Marathon kujiunga na ADEM Jogging Club ili kuendeleza utamaduni wa mazoezi ya mara kwa mara, hatua itakayowasaidia kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

Pia amebainisha kuwa ofisi yake inapanga kuandaa mbio zitakazokutanisha vyuo vyote vilivyopo katika Wilaya ya Bagamoyo kwa lengo la kutangaza utalii. 

Amesema tayari wamekubaliana kuandaa siku maalum ya mbio hizo, ambazo zitaunganisha vyuo vya Bagamoyo na maeneo jirani ili kutangaza vivutio vilivyopo wilayani humo sambamba na kuhamasisha mazoezi.

“Ni muhimu kuwa na mikusanyiko kama hii. Mazoezi ni njia bora ya kuepuka magonjwa, na taasisi nyingi zimekuwa zikitoa wanamichezo wazuri kupitia ushiriki wao kwenye michezo,” amesema Ndemanga.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid, amesema mbio hizo zimefanyika kwa mara ya kwanza na zitakuwa endelevu kwa madhumuni ya kutangaza Bagamoyo na taasisi hiyo kwa wadau mbalimbali.

Amesema ADEM kwa sasa ina miundombinu kongwe inayohitaji ukarabati, na kupitia mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika mara kwa mara, wadau watapata fursa ya kujionea mazingira halisi na kuchangia maboresho.

Aidha, Dkt. Maulid amesema kufanyika kwa mbio hizo pia ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuandaa na kushiriki mbio za aina hiyo.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...