
Balozi wa Palestina nchini, Salim Siam, akizungumza na watendaji wakuu wa Klabu ya Wanahabari ya Dar es Salaam (Dar-PC), Mtendaji Mkuu, Andrew Msechu (kushoto), Naibu Mtendaji Mkuu, Veronica Mrema na Mjumbe wa Bodi, Hamisi Miraji (kulia) wakati alipotembelea ofisi za klabu hiyo kwa ajili ya kujenga mahusiano kati ya ubalozi na klabu.
Balozi wa Palestina nchini, Salim Siam, akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wakuu na waandishi wa habari wa Klabu ya Wanahabari ya Dar es Salaam (Dar-PC) wakati alipotembelea ofisi za klabu hiyo kwa ajili ya kujenga mahusiano kati ya ubalozi na klabu leo Desemba 18. 2025.
Na Mwandishi Wetu
BALOZI wa Palestina anayeiwakilisha nchi yake Tanzania, Salim Siam mapema leo Alhamisi Desemba 18, 2025, amefanya ziara katika Ofisi za Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DAR-PC) akiweka wazi kwamba sasa wamefungua rasmi milango ya ushirikiano na Klabu hiyo kongwe nchini na waandishi wa habari kwa ujumla.
Akiwa katika ziara hiyo Balozi Siam amehimiza wanahabari kuonesha mshikamano na Palestina, ili kupaza sauti ya pamoja kukemea mateso wanayofanyiwa raia wa Palestina na majeshi ya Israel.
Akizungumza baada ya kukutana na viongozi wa DAR-PC katika Ofisi zilizopo Twiga House, Balozi Siam amesema Wapalestina wanahitaji nguvu ya pamoja katika kukemea maovu hasa mauaji yanayoendelea katika eneo la Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, ambayo yamegharimu maisha ya watu wasio na hatia, wakiwemo wanawake na watoto.
Amesema tangu kuanza kwa mashambulizi hayo Oktoba 2023, tayari Wapalestina 70,663 wameuwa kufikia wiki hii ya Desemba 15 mwaka huu, wakiwemo wanahabari 256 na kuharibu kabisa majengo, Barabara, vyanzo vya maji, vyanzo vya nishati, majengo ya hospitali, shule na vyuo.
“Taarifa mpya kutoka kwa Waandishi Wasio na Mipaka inaonesha kuwa kwa mwaka huu wa 2025 pekee kumekuwa na ongeeko la mauaji ya wanahabari kote duniani ambapo kati yao, 67 wameuawa ndani ya mwaka mmoja, karibu nusu yao wakiuawa ndani ya ardhi ya Palestina. Tangu Oktoba 2023 karibu waandishi 220 wa Palestina wameuawa na vikosi vya Israel, ambapo 65 kati ya hao wameuawa wakiwa katika kutekeleza wajibu wao.
“Tunatoa wito kwa wanahabari kutokaa kimya katika mauaji haya ya aina hii, tunawaomba ushirikiano wa dhati katika kuhakikisha ukandamizaji huu unawekwa wazi na kujulikana kote duniani ili kukomesha hali hii,” amesema.
Amesisitiza ofisi yake iko tayari kutoa ushirikiano wa upatikanaji taarifa kuhusu yanayoendelea nchini mwake wakati wote, kwa kuwa anaamini kukandamizwa kwa haki kwa eneo moja ni ukandamizwaji wa haki kwa eneo jingine na kwamba wakandamizaji hao wanapokaliwa kimya hujenga mazoea na kufanya ukandamizaji huo kuwa hali ya kawaida katika maisha ya kila siku.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Wanahabari wa Dar es Salaam (DAR-PC), Andrew Msechu amesema wamekuwa wakifuatilia kwa ukaribu hali ilivyo Palestina na kwamba wanaendelea kuunga mkono msimamo wa Serikali katika kutambua na kuunga mkono upatikanaji wa Dola huru ya Palestina.
Amesema wanahabari wamekuwa wakijionea na kuumizwa na madhila yanayowasibu watu wa Palestina na namna uonevu dhidi ya raia wasio na hatia ulivyokithiri na mara kadhaa wamekuwa wakiangalia namna wanavyoweza kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya uonevu huo.
“Madhila yanayowakabili Wapalestina yanahusisha pia wanahabari, ambao ni sehemu ya jamii pana ya Wapalestina wanaoonewa. Kwa mujibu wa International Federation of Journalists (IFJ), taarifa zinaonesha kuwa kwa mwaka huu wa 2025 pekee, wanahabari 51 wameuawa wakiwa katika juhudi za kupata na kutoa taarifa zinazohusu yanayoendelea nchini mwao. Idadi hii inatisha na sisi kama sehemu ya jamii ya wanahabari tunasikitishwa na kufadhaishwa sana na haya yanayoendelea.
“Wanahabari wetu wamekuwa wakijitahidi kufanya kwa uwezo wao, japo si kwa uzito unaotakiwa kutokana na sababu kadhaa japo tumeendelea kuungana wananchi wa Palestina na jumuiya ya kimataifa kupambana kuhakikisha kunakuwa na Palestina Huru na kwa kutumia kalamu zetu tutahakikisha tunashiriki katika kufanikisha hili,” amesema.
Amesema tatizo ambalo limekuwa likijitokeza mara kadhaa ni kuhusu kupata usahihi wa taarifa, imekuwa si rahisi kuifikia vyanzo sahihi kwa ajili ya kupata taarifa ambazo zinatakiwa kutoka ndani na hivyo kulazimika kudandia taarifa kutoka vyanzo vya kimataifa.
“Tunaamini kwamba sasa, kwa ushirikiano huu wa karibu ulioukoleza leo, ikiwemo hatua hii ya kufika katika ofisi zetu na majadiliano ya kina baina yetu, itakuwa mwanzo mpya wa ushirikiano wenye manufaa kwa ofisi yako, kwa wanahabari na kwa Taifa la Palestina kwa ujumla,” amesema.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...