📍 Dar es Salaam
Tume ya Ushindani (FCC) imefanya semina kwa Mamlaka za Udhibiti Kisekta kujadiliana juu ya masuala ya ushindani kwenye soko.
Akizungumza katika semina hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC Bi. Khadija Ngasongwa amesema kuwa lengo la semina hiyo ni kujadili utekelezaji wa majukumu ya FCC yanayoingiliana na Taasisi hizo za Serikali ili kuhakikisha ushindani unashamiri katika mnyororo wa shughuli za kiuchumi na kumlinda mlaji.
Amesema kuwa hivi karibuni uwekezaji umeongezeka sambamba na maendeleo ya Teknolojia pamoja na mabadiliko ya mifumo ya biashara ambayo yameleta fursa nchini lakini yameibua changamoto mpya katika kudhibiti masoko.
Aidha amesema semina hiyo itajenga uelewa wa pamoja juu kanuni za ushindani na dhima ya kila mdhibiti wa kisekta katika kuhakikisha masoko yanafanya kazi ipasavyo,kukuza ushirikiano kati ya FCC na Wadhibiti wa Kisekta ili kuweza kubadilisha taarifa ,uzoefu na mikakati ya pamoja.
Ameongeza kuwa hii ni fursa kwa Wadhibiti wa Kisekta kukutana na kujadili changamoto zilizopo katika mazingira ya biashara pamoja na kujengeana uwezo kwa wataalamu wetu ili wawe na ujuzi wa kukabiliana na vitendo vya kandamizi na hadaifu sokoni.
Aidha, FCC itahakikisha kuwa ushindani nchini unaendeshwa kwa kuzingatia Kanuni, Sheria na taratibu na haziwezi kutekelezwa na Tume peke yake bila ya uwepo wa wadhibiti wa kisekta kama ambavyo imebainishwa kwenye sheria zinazotusimamia.
Sekta tunazozisimamia zina mchango na uhusiano wa karibu na maslahi ya wananchi hivyo changamoto katika sekta moja zinaweza kuathiri wananchi na Ustawi wa Taifa.
Kilele cha Maadhimisho hayo yaliyobeba kauli mbiu ya "Akili Mnemba (AI), Walaji na Sera za Ushindani" ambayo itafanyika Desemba 5, 2025 katika Hoteli ya King Jada, Jijini Dar es Salaam.
Semina hiyo imefanyika Desemba 03, 2025 katika Ofisi za FCC, Jijini Dar es Salaam
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC Khadija Ngasongwa akizungumza wakati akifungua mkutano wa kujengeana uwezo na Wadhibiti wa Kisekta,jijjni Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC Khadija Ngasongwa akiwa katika picha ya pamoja na Wadhibiti wa Kisekta katika kuelekea Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani yatayofanyika Desemba 5 ,2025 jijini Dar es Salaam.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...