Mgeni rasmi akikata utepea kuashiria uzinduzi wa zahanati hiyo


-Zahanati mpya yazinduliwa katika kijiji cha Mangucha

Wananchi kutoka Mangucha moja ya kijiji kilichopo jirani na mgodi wa dhahabu wa North Mara wilayani Tarime walionekana kuwa na nyuso za furaha na matumaini ya kuondokana na changamoto ya kutembea mwendo mrefu kufuata huduma za afya katika hafla ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kukabidhiwa zahanati ya kijiji ambayo imejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 164 zilizotokana na fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) zilizotolewa na mgodi wa Barrick North Mara unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Ufanikishaji wa mradi huu ni moja ya utekelezaji wa mkakati endelevu wa kampuni ya Barrick unaojumuisha ushirikiano na wadau na vipaumbele ambao umelenga kufanikisha kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii zinazoishi kwenye maeneo yaliyopo Jirani na migodi yake sambamba na kufanikisha utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs).

Akiongea wakati wa hafla ya makabidhiano ya zahanati hiyo Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime, Albinus Kirina, alisema kukamilika kwa ujenzi wa zahanati ya Mangucha kutawaondolea wakazi 4,460 wa kijiji hicho adha waliyokuwa nayo ya kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta huduma za afya nje ya kijiji hicho.


Katibu Tawala wa wilaya ya Tarime (DAS) Saul Mwaisenye, alisema ujenzi wa zahanati hiyo umezingatia viwango vya ubora na thamani ya fedha iliyotumika (value for money). "Nimeridhika na ujenzi wa zahanati hii ndio maana nimekata utepe na kuruhusu Mgodi na Halmashauri kutiliana saini za makabidhiano haya",alisema Mwaisenye akiyemwakilisha Mkuu wa wilaya ya Tarime,Meneja Edward Gowele kama Mgeni Rasmi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, aliitaka idara ya afya kutumia baadhi ya vyumba vya zahanati hiyo kwa ajili ya huduma za wanawake wanaojifungua wakati ujenzi wa majengo ya mama na mtoto na miundombinu ya kichoma taka yakisubiriwa.“Haitakuwa na maana kama akina mama hawatapata huduma za kujifungulia hapa,” alisema Mbunge Waitara.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Matera Newland Chacha, naye aliushukuru Mgodi wa Barrick North Mara na kuahidi kuendelea kuupatia ushirikiano katika utekelezaji wa miradi mingine ya CSR ndani ya halmashauri hiyo.


Naye Diwani wa Kata ya Nyanungu, Tiboche Richard, aliishukuru Barrick North Mara kwa kuwezesha ujenzi wa zahanati hiyo ambayo imesogeza huduma za afya jirani na wananchi wa Mangucha.“Tunawashukuru sana watu wa Mgodi wa Barrick North Mara na tutaendelea kuwa mabalozi wazuri wa mgodi,” alisema Diwani Tiboche.


Awali, Meneja Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, alisema afya ni moja ya sekta ambazo wanazipa kipaumbele kwenye utekelezaji wa miradi inayogharimiwa na fedha za mpango wao wa CSR.Francis Uhadi


"Sekta ya afya ni ya pili kwa ukubwa wa uwekezaji wa CSR, ikiwa na asilimia 20 ya fedha zote tulizowekeza hadi sasa. Tangu mwaka 2020 hadi sasa, mgodi umewekeza shilingi bilioni 5.4 katika ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, nyumba za watumishi na vifaa tiba.


"Kwa mwaka 2025, tunatekeleza miradi 21 ya afya yenye thamani ya shilingi bilioni 2.4. Miradi mingi ipo kwenye hatua za mwisho, ikiwemo huu wa Zahanati ya Mangucha uliokamilika kwa asilimia 100, na mingine itaendelea kukabidhiwa kwa halmashauri kadiri inavyokamilika.


“Makabidhiano ya zahanati hii ni ushahidi wa mafanikio tunayoyapata kupitia utekelezaji wa miradi ya CSR kwa ushirikiano wa karibu kati ya Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime pamoja na wananchi kwa ujumla,” alisema Uhadi.


Akizungumza kwa niaba ya wana-Mangucha, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Kemahi Irumbe Mgesi,alitoa shukrani kwa kujengewa zahanati hiyo na aliahidi kushirikiana na wananchi kulinda miundombinu yake kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Ripoti ya utekelezaji Mkakati Endelevu ya mwaka 2024 ya kampuni ya Barrick Mining Corporation iliyotolewa karibuni imebainisha mafanikio muhimu yaliyopatikana katika uendeshaji wa shughuli zake katika mataifa mbalimbali duniani.


Mafanikio muhimu endelevu yaliyopatikana yaliyobainishwa katika ripoti hiyo ni kampuni kuwekeza katika matumizi ya vyanzo vya nishati mbadala, Uwezeshaji biashara katika maeneo yake ya kazi,miradi ya jamii na Serikali, na kuunda ushirikiano na jamii zinazoishi Jirani na maeneo yake ya kazi kwa kutekeleza miradi ya kujenga shule,vituo vya afya, upatikanaji wa maji safi ya kunywa na miundombinu mingine muhimu-pamoja na uwekezaji katika kuwezesha upatikanaji wa walimu bora, wauguzi na vifaa vinavyohitajika kuboresha upatikanaji wa huduma hizi.
Zoezi la kusaini na kukabidhiana nyaraka za jengo la Zahanati kati ya mgodi wa Barrick North Mara na Halmashauri ya Tarime VijijiniMbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara akizungumza wakati wa hafla hiyo

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Matera Newland Chacha akizungumza kwenye hafla hiyo

Afisa Mahusiano wa Barrick North Mara,Hermence Christopher akiongoza utaratibu wa ratiba katika hafla hiyo.
Muonekano wa sehemu ya nyuma ya jengo la Zahanati mpya ya Kijiji cha Mangucha
Sehemu ya wananchi wakiwemo viongozi wa serikali za vijiji kata ya Nyanungu

Katibu Tawala wa wilaya ya Tarime (DAS) Saul Mwaisenye akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya zahanati hiyo



Viongozi wakikagua jengo la zahanati hiyo


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...