Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
JAMII imetakiwa kuwa mstari wa mbele katika kufuatilia, kutambua na kuchangamkia fursa mbalimbali za maendeleo zinazotolewa na Serikali ili kujikwamua kiuchumi na kijamii, sambamba na kutimiza malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo na fursa kwa makundi maalum kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Akizungumza na waandishi wa habari,jijini Dar es Salaam leo Desemba 22, 2025 Dkt. Gwajima amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka vipaumbele vinavyolenga kujenga Taifa jumuishi kwa kuwekeza katika sekta zinazoajiri watu wengi ikiwemo kilimo, utalii, viwanda, ujenzi, michezo, sanaa za ubunifu na madini, hatua itakayoongeza fursa za kiuchumi kwa wanawake, vijana, wazee na makundi mengine maalum.
Waziri huyo ametoa wito kwa wananchi kutumia vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru ili kupata ujuzi na maarifa yatakayowawezesha kujiajiri, kuajiriwa na hata kuajiri wengine, akisisitiza kuwa elimu ya vitendo ni nyenzo muhimu ya mabadiliko ya maisha ya jamii.
Katika kuimarisha ustawi wa jamii, Dkt. Gwajima amesisitiza umuhimu wa malezi bora ya watoto kwa ushirikiano wa wazazi wote wawili, akieleza kuwa Serikali imeendelea kutoa elimu ya malezi kupitia miongozo na programu maalum ikiwemo programu ya Furaha Teen inayotekelezwa kwa majaribio katika mikoa ya Songwe na Mbeya.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi na programu za kijamii zinazohusu hifadhi ya jamii, afya ya akili, ushauri nasaha, ulinzi wa watoto na wazee, pamoja na usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia, hatua iliyosaidia kupunguza migogoro na kuimarisha mshikamano wa kifamilia.
Kuhusu ustawi wa wazee, Waziri Gwajima amesema Serikali imeendelea kutoa huduma za msingi ikiwemo chakula, malazi, matibabu na bima ya afya bila malipo, huku zaidi ya wazee milioni 1.2 wakinufaika na vitambulisho vya matibabu, sambamba na kuanzishwa kwa Mabaraza ya Wazee nchini kote kama jukwaa la ushauri na urithishaji wa maadili mema kwa jamii.
Katika eneo la uwezeshaji kiuchumi, Serikali imeendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wafanyabiashara ndogondogo, hususan vijana na wanawake, kupitia Benki ya NMB pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF), huku maelfu ya wananchi wakinufaika na mikopo hiyo kwa ajili ya kukuza biashara na kuongeza kipato.
Vilevile, Dkt. Gwajima amehimiza jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na dhidi ya watoto, akibainisha kuwa kampeni za kijamii na ushirikiano na wadau mbalimbali zimewezesha matukio mengi ya ukatili kuripotiwa na kushughulikiwa.
Waziri huyo amesisitiza kuwa maendeleo jumuishi yanahitaji ushiriki wa jamii kwa ujumla katika kutumia fursa za kiuchumi, kijamii na kisiasa zinazotolewa na Serikali, huku akisisitiza kuwa amani, uzalendo, maadili mema na bidii ni msingi muhimu wa kufikia ustawi wa Taifa. Amevitaka vyombo vya habari kuendelea kuwa daraja kati ya Serikali na wananchi ili taarifa sahihi ziwafikie walengwa kwa wakati.


.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...