Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

UJENZI wa kitengo cha kutoa huduma za kinywa na meno katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Kampasi ya Mloganzila unatajwa kuwa miongoni mwa miradi itakayowawezesha wananchi kujivunia na kunufaika na huduma za tiba zitakazotolewa na Kituo cha Umahili cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kinachojengwa katika eneo hilo.

Serikali imesema kituo hicho kitawezesha utoaji wa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu pamoja na huduma za kinywa na meno kwa wagonjwa wa ndani na wale kutoka nje ya nchi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema hayo leo Desemba 17, 2025 , wakati alipofanya ziara ya kikazi kukagua miundombinu inayotekelezwa na chuo hicho kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), kwa lengo la kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo.

Profesa Mkenda amesema Kampasi ya Mloganzila inatarajiwa kuwa kitovu kikubwa cha taaluma za kitabibu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku sekta ya afya ikichukua nafasi muhimu katika maendeleo ya eneo hilo.

Amesema eneo hilo linaonyesha ukubwa wa uwekezaji uliofanyika kuanzia hospitali iliyopo hadi kituo cha umahili cha Afrika Mashariki cha magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, ambacho kinatekelezwa kwa makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Alifafanua kuwa wagonjwa na wataalamu kutoka nchi wanachama watapata huduma katika kituo hicho kwa gharama nafuu, hatua itakayosaidia pia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi.

Ameongeza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki tayari imekubaliana kujenga kituo kingine cha umahili kitakachotoa huduma za kinywa na meno katika eneo hilo hilo, sambamba na ujenzi wa vituo vingine vitakavyosaidia kuimarisha tafiti na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya.

Aidha, Profesa Mkenda ameeleza kuwa suala la kuwapeleka vijana kusoma, hususan katika nyanja za sayansi, teknolojia na utafiti, linapaswa kuzingatia fursa zilizopo ikiwemo ufadhili wa masomo kama Samia Scholarship katika maeneo ya nyuki na sayansi kwa ujumla.

Amesema idadi kubwa ya vijana wameonyesha umahiri katika masomo ya sayansi, jambo linalotoa fursa ya kuendelea na elimu ya juu katika maeneo yenye mwelekeo wa utafiti, akisisitiza kuwa jukumu kubwa la elimu ya juu ni kufanya tafiti zinazoendana na changamoto zilizopo katika jamii.

Ameongeza kuwa tafiti hizo zinapaswa kujikita katika mazingira husika na changamoto za kiafya zilizopo, badala ya kunakili tafiti kutoka maeneo mengine ambayo hayalingani na uhalisia wa ndani.

Profesa Mkenda amesema bado kuna dawa nyingi za asili ambazo hazijafanyiwa majaribio ya kitabibu licha ya kuwepo kwa ushahidi kutoka kwa watumiaji wanaoeleza kupata nafuu, akisisitiza umuhimu wa kujikita katika tafiti hizo ili kuisaidia serikali.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Apollinary Kamuhabwa, amesema wananchi wanapaswa kutarajia kuongezeka kwa ubora na weledi wa wataalamu watakaohitimu chuoni hapo, pamoja na kuanzishwa kwa programu mpya katika maeneo yenye uhaba wa wataalamu, hatua itakayoongeza mchango wa chuo katika sekta ya afya.

Amesema Serikali imetoa dola za Marekani milioni 45.5 kwa ajili ya mradi huo, ambapo dola milioni 30 zimeelekezwa Kampasi ya Mloganzila na dola milioni 15 Kampasi ya Kigoma. Alifafanua kuwa Mloganzila kunajengwa mabweni ya wasichana, maabara 20, jengo la kuhifadhi miili ya binadamu kwa ajili ya mafunzo, jengo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, maktaba, jengo la utawala pamoja na miundombinu mingine.

Profesa Kamuhabwa almeeleza kuwa hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 50 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2026, akibainisha kuwa ni uwekezaji mkubwa utakaoimarisha uwezo wa chuo kutoa huduma za ubobezi katika taaluma za afya na kuzalisha wataalamu wengi zaidi.

Ameongeza kuwa kituo cha umahili cha magonjwa ya moyo na mishipa ya damu tayari kimekamilika, na mwaka ujao ujenzi wa hospitali ya magonjwa ya kinywa na meno utaanza kwa kuwa fedha tayari zimetengwa. Alisema miundombinu yote itajengwa katika eneo lenye ukubwa wa hekari 380, na hivyo kufanya Mloganzila kuwa kituo kikubwa cha umahili wa mafunzo na taaluma za afya mara baada ya kukamilika kwa awamu hii.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda (wa kwanza kushoto), akipatiwa maelezo na Mshauri Elekezi kutoka Arqes Africa, Bi. Neema Mbwambo (wa pili kulia), kuhusu maendeleo ya mradi wa ujenzi wa mabweni ya wanafunzi, madarasa ya kufundishia, maabara za kisasa, maktaba na jengo la utawala katika Kampasi ya Mloganzila, wakati wa ziara ya kikazi iliyofanyika leo, Desemba 17, 2025, katika Kampasi hiyo, Dar es Salaam. Katikati ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. Appolinary Kamuhabwa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa HEET katika Kampasi ya Mloganzila, MUHAS, Dar es Salaam




Wafanyakazi wa MUHAS pamoja na wasimamizi wa mradiwa HEET wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Prof. Adolf Mkenda
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...