MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeanza mafunzo maalum ya usimamizi wa miradi ya maendeleo kwa ngazi ya menejimenti, yanayolenga kuimarisha utekelezaji wa miradi ya uwekezaji wa miundombinu (Capital Expenditure – CapEx), ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini.

Mafunzo hayo, yanayoendeshwa na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yamefunguliwa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Ladislaus Chang’a, na yanatarajiwa kuhitimishwa Disemba 19, 2025.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Dkt. Chang’a alisema TMA, kama taasisi ya Serikali iliyopewa dhamana ya kutoa huduma za hali ya hewa pamoja na kuratibu na kudhibiti shughuli zote zinazohusiana na masuala ya hali ya hewa nchini, inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayochangia majukumu yake ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Alifafanua kuwa miongoni mwa miradi inayotekelezwa na TMA ni ile ya uwekezaji wa miundombinu (CapEx), ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Ufuatiliaji wa Matukio ya Tsunami (Tsunami Centre), pamoja na mradi wa SOFF unaofadhili ujenzi wa vituo vipya vitatu (3) vya kupima hali ya hewa katika anga za juu.

“Miradi hii inahitaji usimamizi thabiti, uwajibikaji na ufanisi mkubwa ili iweze kuleta tija inayotarajiwa kwa Taifa. Mafunzo haya ni muhimu katika kujenga uwezo wa menejimenti kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango na kwa wakati,” alisema Dkt. Chang’a.

Kwa upande wake, Mtiva wa Kitivo cha Mafunzo ya Insia na Sayansi za Jamii wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Dkt. Leticia Rwabishungi, aliishukuru TMA kwa kuchagua IAA kuwa mshirika katika mafunzo hayo, akisema chuo kina wigo mpana wa kozi mbalimbali katika ngazi tofauti, siyo uhasibu pekee.

“IAA iko tayari kuendelea kushirikiana na taasisi za umma na binafsi katika kuwajengea uwezo watumishi kupitia mafunzo yenye mwelekeo wa vitendo na mahitaji halisi ya soko,” alisema Dkt. Rwabishungi.

Ufunguzi wa mafunzo hayo ulihudhuriwa na viongozi na wataalamu mbalimbali wakiwemo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri wa IAA, wajumbe wa menejimenti ya TMA, wakufunzi kutoka IAA, pamoja na wataalamu kutoka TMA, IAA na UNDP.

Mafunzo haya yanatarajiwa kuongeza ujuzi na weledi wa menejimenti ya TMA katika kupanga, kusimamia na kutathmini miradi ya maendeleo, hatua inayochangia kuimarisha mifumo ya tahadhari ya mapema na huduma bora za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu ya nchi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...