Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Abdallah Mwaipaya, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, amesema hayo wakati wa hafla ya kuhitimisha mbio za Utumishi Marathoni 2025 zilizoandaliwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Kampasi ya Mtwara.
Akiwasilisha salamu za Mkuu wa Mkoa, Mhe. Mwaipaya amesema, “Historia ya Chuo cha Utumishi wa Umma ni sehemu muhimu ya mafanikio ya utumishi wa umma nchini. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000, chuo hiki kimekuwa mhimili muhimu wa kutoa elimu, mafunzo, na ujuzi unaowawezesha watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu, na ufanisi.”
Pia, Mhe. Mwaipaya amepongeza Chuo kwa maandalizi mazuri ya tukio hili na kusema kuwa mbio za marathoni si tu zinaboresha afya na mshikamano, bali pia zinaunda hisia za uzalendo na utu miongoni mwa washiriki. Ameongeza kuwa, “Marathon hii si tukio la michezo tu; ni kumbukumbu hai ya safari ndefu na mafanikio makubwa ambayo chuo chetu kimeipitia kwa kipindi cha miaka 25. Amessitiza kuwa, safari ya miaka ishirini na tano imejengwa juu ya misingi ya nidhamu, ubunifu, ushirikiano, na kujituma kwa manufaa ya taifa letu.”
Naye Makamu Mkuu wa Chuo -Taaluma, Tafiti na Shauri za Kitaalam, Dkt. Hamisi Amani, aliyemwakilisha Mkuu wa Chuo na kuwa Mtendaji Mkuu, amesema kuwa safari ya miaka 25 ya chuo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 ni jambo la kujivunia.
“Leo si tu tunakimbia kwa ajili ya afya na umoja, bali tunasherehekea mafanikio, historia, na mchango mkubwa wa chuo kwa taifa letu kwa takribani robo karne,” amesema Dkt. Amani.
Ameongeza kuwa tangu kuanzishwa kwake, Chuo kimepata maendeo makubwa na mabadiliko chanya katika utoaji wa elimu, uboreshaji wa huduma, na katika kuimarisha uwezo wa watumishi wa umma nchini.
Dkt. Amani amesema kuwa, mafanikio yaliyopatikana nia ni pamoja na kupanuka kwa kampasi kutoka mbili hadi sita, kuongezeka kwa kozi na programu za muda mrefu, kuboreshwa kwa mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi wa umma na matumizi yaa teknolojia katika kutoa mafunzo jambo liliwezesha chuo kuwafikia watumishi wa umma wengi kwa urahisi.


.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...