Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itachukua hatua kali za kisheria dhidi ya viongozi na watumishi wa umma watakaoshindwa kujaza na kuwasilisha kwa wakati fomu za tamko la maadili katika Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa kauli hiyo leo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Zanzibar, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Dimani, Mkoa wa Mjini Magharibi. Amesisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria, kila kiongozi na mtumishi wa umma anatakiwa kuwasilisha fomu hizo kabla ya tarehe 30 Desemba 2025.
Akielezea taarifa ya Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa hadi sasa ni viongozi 530 pekee, sawa na asilimia 19, kati ya viongozi 2,750 wanaotakiwa kisheria, ndio waliokamilisha zoezi hilo. Ameeleza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya watakaokiuka matakwa hayo ya kisheria.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali ipo katika maandalizi ya kuanzisha Mfumo wa Upimaji wa Utendaji Kazi kwa Viongozi, utakaolenga kuongeza uwajibikaji, ufanisi na tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kuimarisha utendaji wa taasisi za umma.
Akizungumzia mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu wa uchumi, Rais Dkt. Mwinyi amesema Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi (ZAECA) imepokea na kufanyia kazi jumla ya taarifa 524. Amefafanua kuwa katika kipindi cha Januari hadi Oktoba 2025, ZAECA imefanikiwa kidhibiti na kuokoa Jumla ya Shilingi 6,426,282,551/= na dola za kimarekani (USD) 89,371 zilirejeshwa Serikalini na shilingi 1,143,487,556/= na dola za Kimaekani (USD) 4,999 zilirejeshwa kwa wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Tanzania, ikiwemo Zanzibar, imeendelea kupiga hatua kubwa katika utekelezaji wa Malengo ya Umoja wa Mataifa yanayohusiana na haki za binadamu na mapambano dhidi ya rushwa, kupitia uridhiaji na utekelezaji wa mikataba na mikakati ya kimataifa.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa viongozi wa taasisi za Serikali kutumia vyombo vya habari kuwaelimisha wananchi kuhusu shughuli na maendeleo ya nchi, na pia kuhimiza wananchi, vyombo vya habari, asasi za kiraia na sekta ya umma kushirikiana na Serikali katika kuimarisha utawala bora, haki za binadamu na mapambano dhidi ya rushwa.
Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu uvunjaji wa maadili ya viongozi, ambapo jumla ya malalamiko 28 yalipokelewa na manane tayari yamefanyiwa kazi.

















Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...