Farida Mangube Morogoro.
Serikali, kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeeleza wazi kuwa haitegemei kuona migogoro ya ardhi ikiongezeka nchini, bali inaongeza nguvu katika kushughulikia migogoro iliyopo na kuhakikisha rasilimali ardhi zinatumiwa kwa usimamizi thabiti.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard G. Akwilapo, wakati kwenye Mahafali ya 44 ya Chuo cha Ardhi Morogoro ambapo amesisitiza kuwa Serikali inajipanga kuongeza teknolojia katika usimamizi wa ardhi, kuendeleza uwezo wa wataalamu, kuboresha mifumo ya sekta hiyo na kuhakikisha ardhi inatumiwa kwa njia bora, huku akibainisha kuwa ardhi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bw. Mussa Kilakala, amebainisha kuwa Chuo cha Ardhi Morogoro kimekuwa na mchango mkubwa katika utatuzi wa migogoro ya ardhi huku akisifu chuo hicho kimekuwa kitovu cha kutengeneza wataalamu wa ardhi waliokidhi mahitaji ya Serikali na jamii,
huku pia kikichangia katika kuongeza ufanisi wa mipango ya kitaifa ya ardhi. Bw. Kilakala aliongeza kuwa elimu inayotolewa na chuo hiki inasaidia kupunguza pengo la wataalamu nchini na kuandaa nguvu kazi yenye weledi inayoweza kushughulikia changamoto za ardhi zinazojitokeza.
Bw. Charles Saguda ni Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro, amebainisha kuwa chuo kimefanikisha miradi kadhaa ya kitaaluma ikiwemo ujenzi wa madarasa matatu katika kampasi kuu, kuanzisha Mpango Kabambe wa Chuo (2023–2043) unaolenga kuongeza udahili wa wanafunzi, kuboresha miundombinu, kuongeza idadi ya kozi, na kuimarisha mazingira ya tafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia.
Aidha Bw. Saguda alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na wadau, serikali na familia za wahitimu ili kuhakikisha chuo kinaendelea kuwa kitovu cha kutoa wataalamu wa hali ya juu katika sekta ya ardhi.
Kwa mwaka wa masomo 2024/2025, Chuo cha Ardhi Morogoro kimeadhimisha mahafali ya 44 ambapo wahitimu 450 walitimiza masomo yao wakiwemo Jiomatikia (Upimaji Ardhi) 272, Upangaji Miji na Vijiji 155, na Mifumo ya Taarifa za Kijiografia (GIS) 23, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kozi ya GIS kuhitimisha.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...