TAASISI ya Series Foundation ikishirikiana na Klabu ya Lions International Tanzania imetoa jumla ya vifaa 150 vinavyojumuisha soksi, kofia na magauni katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Dar es Salaam kwa ajili ya mama aliyejifungua na watoto walio chini ya miezi mitatu.

Akizungumza wakati wa kutoa msaada huo Desemba mosi, 2025 Afisa Mtendaji Mkuu wa Seris Foundation, Deborah Wammi amesema moja ya jukumu lao ni kuangalia hali ya mama na mtoto ambaye yuko chini ya miezi mitatu na kumpatia huduma.

Amesema wamefika hospitalini hapo kwa ajili ya kufanya matendo mema kwa kuwapatia zawadi ya siku ya leo. "Mbali na hilo tumeweza kutoa magauni 50 yanayovaliwa na wagonjwa waliolazwa kwa kufanyiwa upasuaji na wale waliolazwa kawaida zawadi za leo ni za watoto na magauni haya yatatumika kadri siku zinavyokwenda kwa wanaojifungua kwa njia zote na tumefanya hivi ili kutimiza moja ya malengo yetu kwa kugusa watoto chini ya miezi 3 na mama," amesema.

Wammi amesema wamepeleka pampasi 50, soksi na kofia 50 idadi ambayo walipewa na hospitali kutokana na wastani wa watoto 20 hadi 25 ambao huzaliwa kwa siku moja.

Ametoa wito kwa taasisi zingine kutoa huduma katika mazingira yanayowazunguka badala ya kwenda mbali ilhali karibu kuna changamoto za aina hiyo. "Natoa wito tuendelee kuwatembelea watoto wanaozaliwa kwa sababu wanachangamoto nyingi na familia zao zinahudumia lakini ukija kama taasisi unakuwa umegusa maisha yao moja kwa moja," amesema.
Shuwaa Omary Kaniki ni Muuguzi Kiongozi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja amesema leo wamepokea ufadhili kutoka Seris Foundation ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani. "Kuchagua eneo hili upande wa mama na mtoto ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika ujenzi wa hospitali na huduma za mama na mtoto hivyo basi tunashukuru kwa zawadi hizi ambazo ni nguo kwa ajili ya wagonjwa, kofia za watoto, soksi za watoto pamoja na pampasi tunawashukuru sana kwa moyo wao wa kujitolea na kutuchagua sisi Mnazi Mmoja kama sehemu ya kujumuika nao katika maadhimisho haya," amesema.

Amesema bado wanahitaji vifaa vingi ambavyo ni endelevu ikiwemo monitor kwa ajili ya uangalizi wa karibu mgonjwa anapofanyiwa upasuaji pamoja na vifaa vya kumuangalia mama anapokuwa kwenye uchungu ili kutambua mapigo ya moyo ya mtoto yapo katika hali gani kwa wakati huo.

Sambamba na hilo amesema upande wa wodi ya watoto wachanga wenye changamoto ambapo mashine kwa ajili ya kusaidia watoto wachanga zaidi inahitajika na nyingine kwa ajili ya kuwa monitor hali zao wanapokuwa kwenye matibabu.

Naye Bakary Omary, mwanachama wa Klabu ya Lions International Tanzania, ametumia fursa hiyo kuyataka mashirika na taasisi nyingine kuiga mfano huo kwa kuendelea kuisaidia jamii, hususan kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa kama sekta ya mama na mtoto. "Sisi Tanzania ni ndugu na matatizo tuliyonayo ni lazima tuyakabili pamoja na kwa nguvu moja kwa sababu serikali siku zote imekuwa ikijitahidi kufanikisha hilo lakini sisi kama wadau tunawajibu wa kuongeza mchango kwenye jitihada hizo ili jamii iweze kunufaika," amesema.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...