Na Said Mwishehe,Michuzi TV


TAASISI ya Uongozi imezindua programu ya Mafunzo ya Viongozi Chipukizi ambapo lengo kuu ni kuendeleza viongozi nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla ili wawe bora watakapokuja kushika nafasi za juu katika uongozi.

Akizungumza leo Desemba 11,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa programu ya Mafunzo ya Viongozi Chipukizi, Naibu Waziri Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Regina Qwaray amesema anawapongeza Taasisi ya Uongozi kwa kubuni na kuandaa programu hiyo muhimu kwa kwa viongozi na taifa kwa ujumla.

“Nchi zote duniani zina jukumu la kuandaa na kuwaendeleza viongozi. Jukumu hili la kuandaa viongozi limekua na umuhimu zaidi hususani katika mazingira ya sasa yanayobadilika kwa kasi…

“Na hivyo kulazimu viongozi wawe na uwezo na ujuzi wa kufanya maamuzi ya kimkakati, kutatua changamoto, kuhamasisha wanaowaongoza, na kutumia teknolojia kuimarisha utendaji kazi.

“Kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kuwa kuishi ni kujifunza, na kujifunza ni kujaribu kuweka mazingira ya kuishi vizuri zaidi. Hili ni kweli hata kwenye uongozi.”

Ameongeza ili uwe kiongozi bora na kuongoza vizuri, ni lazima uendelee kujifunza kila siku ili kukabiliana na changamoto za kiuongozi ikiwemo kubuni mbinu mbalimbali za kusimamia mabadiliko ya kimfumo, kiutawala, kiuchumi, kiteknolojia na kitamaduni yanayojitokeza kila siku.

Kuhusu dhumuni la programu ya Mafunzo ya Viongozi Chipukizi amesema itachangia kuandaa viongozi wenye sifa za ubunifu, uadilifu, uaminifu na uwezo wa kutekeleza kwa ufanisi mipango ya maendeleo.

Pia itasaidia Serikali kuwa na viongozi watakao timiza matarajio ya wananchi. “Nina imani kuwa maarifa na ujuzi utakaotolewa kwa washiriki wa programu hii utawapa msingi bora na utayari kuongoza na kutoa huduma bora kwa wanachi.”

Akieleza zaidi amewaambia washiriki wa programu hiyo wapatao 30 kuwa kama viongozi, wanatakiwa kuongoza kwa ufanisi na kutatua changamoto zinazowazunguka.

“Ushauri wangu kwenu changamoto ni sehemu ya uongozi; wakati mwingine hata mafanikio ya leo yanaweza kuwa changamoto za kesho. Hivyo, huwezi kuepuka changamato kama binadamu, na zaidi kama kiongozi.

“Kazi kubwa ni kuhakikisha tunashirikisha wenzetu katika utatuzi wa changamoto ili kuja na masuluhisho ya pamoja na kuandaa mikakati ya pamoja ya utekelezaji.”

Pamoja na hayo amesema kwa viongozi ni muhimu kutambua uwezo na udhaifu wake kwani hiyo itakusaidia kubaini maeneo anayohitaji kuyafanyia kazi ili kukuza mustakabali wa maendeleo yake katika uongozi.

“Hii ndiyo sababu ya msingi ya programu hii kuanza na utambuzi wa uwezo na udhaifu wa washiriki ili kubaini maeneo ya kufanyia kazi wakati na baada ya mafunzo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi Kadari Singo amesema wameona iko haja ya kuwa na programu ambayo lengo lake ni kuwaandaa viongozi mapema ili baadae wawe bora.

“Wanasema samaki mkunje angali mbichi hivyo tumeona kwamba tukianzisha programu ya viongozi chipukizi itawaandaa mapema sana hawa viongozi wakati wanapofika nafasi za ngazi za juu wanakuwa wameshajengwa ipasavyo

“Kwasasa tumeanza na viongozi Chipukizi wa Tanzania na baadae baada ya miaka miwili au mitatu tutakuwa na viongozi kutoka mataifa mengine kama ilivyo katika programu zetu nyingine ambapo tunaviongozi wa mataifa mengine.”

Aidha amesisitiza lengo la programu hiyo ni kuwawezesha viongozi chipukizi kutambua vipaji vyao wakiwa wadogo lakini pili wasiishi kwa kujifunza makosa kwasababu makosa mengine unakuwa nayo mpaka unashika nafasi ya juu unakuta huwezi kuyarekebisha tena, yameshakuwa sugu katika maisha yako.

“Sasa kupitia programu hii tunataka mapema kabisa viongozi wetu tuwapatie zana za kufanyia kazi ambazo zitawafanya wawe viongozi bora na kwamba mafunzo hayo ni ya miezi sita,” amesema Singo.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Regina Qwaray akizungumza leo Desemba 11,2925 jijini Dar es Salaam wakati wa wakati wa uzinduzi wa programu ya Mafunzo ya Viongozi Chipukizi .








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...