NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

WAFANYABIASHARA wanaojihusisha na uuzaji wa maziwa nchini wametakiwa kujisajili katika Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) ili kupata idhini ya kisheria ya kufanya biashara hiyo, huku wakionya kuwa kufanya shughuli hizo bila usajili ni kinyume cha sheria.

Wito huo umetolewa leo Desemba 23, 2025 jijini Dar es Salaam na Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, George Msalya, wakati wa kikao kazi cha mwaka kinachowakutanisha wadau wa tasnia ya maziwa nchini.

Msalya amesema kupitia Sheria ya Maziwa namba 8 ya mwaka 2004, Bodi ya Maziwa imepewa mamlaka ya kisheria kuwaondoa au kuwachukulia hatua watu wanaojihusisha na biashara ya maziwa bila kufuata taratibu zilizowekwa, hatua inayolenga kudhibiti madhara yanayoweza kujitokeza kwa walaji na uchumi wa Taifa.

Ameeleza kuwa wafanyabiashara wanaweza kujisajili kwa urahisi kupitia tovuti ya Bodi ya Maziwa kwa kubofya kiungo kinachowaelekeza kwenye mfumo wa MIMS (Milk Industry Management Information System), hatua itakayowasaidia kuepuka adhabu ikiwemo kufungiwa biashara.

Msalya ametaja baadhi ya vigezo vya usajili kuwa ni pamoja na kumiliki ghala la kuhifadhia maziwa kwa wasindikaji, pamoja na kuwa na shamba la mifugo linalotambulika kisheria kwa wazalishaji wa maziwa.

Kwa upande wake, Afisa Masoko wa Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza kupitia kiwanda chake cha uzalishaji maziwa Kingolwira-Morogoro (Prisons corpation sole), Glorious masawe amesema mikutano hiyo ya mwaka ni muhimu kwa wadau kwani imekuwa ikiongeza weledi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Mwaka jana tulishiriki kwa mara ya kwanza na tukapata tuzo ya mzalishaji bora wa maziwa ya daraja la kwanza. Ushiriki wetu katika kikao hiki unatupa mwanga wa kujua maeneo ya kuimarisha nguvu na yale yanayohitaji maboresho katika mnyororo wetu wa thamani,” amesema Bi. Glorius.

Naye Afisa Viwango kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Zena Issah, amesema TBS imekuwa ikishiriki kikamilifu katika maandalizi ya Wiki ya Maziwa 2026 ili kuhakikisha uzalishaji wa maziwa bora na salama unazingatiwa, jambo ambalo ni muhimu kwa afya ya mlaji na maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Kwa mujibu wa takwimu, sekta ya maziwa imechangia asilimia mbili ya pato la Taifa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, ikiwa ni chachu muhimu ya shughuli za kiuchumi nchini.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...