WAHITIMU 1,362 wa ngazi mbalimbali za masomo ya afya na sayansi shirikishi wametunukiwa vyeti na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) katika Mahafali ya 19 yaliyofanyika leo Desemba 4, 2025 jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa chuo hicho, Prof. David Homeli Mwakyusa, aliwapa wahitimu hao vyeti vinavyohusisha stashahada, shahada ya kwanza, shahada za uzamili, digrii za ubobezi na digrii za uzamivu, hatua inayotoa mchango mpya katika kuimarisha sekta ya afya nchini.

Akizungumza katika mahafali hayo, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa, alisema wanawake ni 504, ambayo ni asilimia 37 ya wahitimu wa mwaka huu. Alifafanua kuwa stashahada ya juu imetolewa kwa wahitimu 108, shahada ya kwanza kwa 680, shahada za uzamili 511, digrii za ubobezi 54, huku wahitimu tisa wakikamilisha digrii ya uzamivu ya udaktari wa falsafa.

Prof. Kamuhabwa alisema MUHAS imeendelea kuimarisha uwekezaji katika TEHAMA kwa ajili ya mazingira bora ya ufundishaji, ujifunzaji, utafiti na utawala. Kwa mwaka 2025, chuo kiliboresha miundombinu na mifumo ya kidijitali, ikiwamo usimikaji wa Government Service Directory (GSD) na mGov Platform kwa ushirikiano na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Akizungumzia utafiti, alisema chuo kimeratibu miradi 121 kwa mwaka wa masomo 2024/2025, ishara ya kukua kwa ubunifu na mchango wa MUHAS katika maendeleo ya Taifa. Machapisho ya kitaaluma pia yameongezeka kutoka 324 hadi 577 kwa mwaka 2024/2025, huku bunifu 96 za wanafunzi na watumishi zikiendelezwa kwa lengo la kuzifikisha sokoni kupitia ushirikiano na sekta ya viwanda na biashara.

Alibainisha pia kuwa MUHAS imeanzisha Mfuko wa Maendeleo wa Ali Hassan Mwinyi (AHMMETF) kwa ajili ya kufadhili tafiti, ubunifu na elimu ya afya kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Dkt. Harrison Mwakyembe, alisema Baraza limeendelea kuongoza maendeleo ya chuo kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, uwajibikaji, usawa wa kijinsia na matumizi ya teknolojia. Aliongeza kuwa chuo kimeanzisha mitaala mipya 14 ya shahada ya kwanza na uzamili ili kukidhi mahitaji ya sasa ya sekta ya afya ndani na nje ya nchi.

Amesema pia kuwa programu 11 za uzamili na ubobezi zimekusudiwa kuzalisha wataalamu bobezi watakaokuza huduma za kibingwa nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki, kama sehemu ya mkakati wa kuendeleza utalii tiba.

Aidha, Dkt. Mwakyembe alisema MUHAS inaendelea kutoa ushauri kwa Serikali katika maeneo ya magonjwa yasiyoambukiza, afya ya akili, huduma za mama na mtoto na maboresho ya mitaala ya uuguzi ili kuongeza ubora wa wauguzi nchini.

Baadhi ya wahitimu, akiwemo Jackline G. Malavanu na Alfred Chibwe, walilishukuru chuo kwa kuwapatia elimu bora na kuwaandaa kitaaluma kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. David Homeli Mwakyusa  akiwatunuku wahitimu wa digrii za ubobezi na digrii ya uzamivu katika Mahafali ya 19 ya MUHAS yaliyofanyika leo Desemba 4, 2025 jijini Dar es Salaam
Makamu Mkuu wa MUHAS Prof. Appolinary Kamuhabwa akitoa taarifa ya utendaji wa chuo katika Mahafali ya 19 ya MUHAS yaliyofanyika leo Desemba 4, 2025 jijini Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Baraza la MUHAS , Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza katika Mahafali ya 19 ya MUHAS.
Makamu Mkuu wa taaluma  MUHAS Prof. Emmanuel Balandya akizungumza katika Mahafali ya 19 ya Chuo hicho.
Mwakilishi wa wahitimu  wa Shahada za  Uzamili MUHAS Alfred Chibwe akitoa hotuba

Baadhi ya wahitimu wa Chuo MUHAS wakishangilia baada ya kutunikiwa stashahada, shahada ya kwanza, shahada za uzamili, digrii za ubobezi na digrii ya uzamivu.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...