NA MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya Udalali ya Yono Auction Mart, imetoa siku 14 kwa wananchi , taasisi na vikundi waliokopa katika Mfuko wa Pembejeo (AGITF) nchini kurejesha fedha hizo kabla ya kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufirisiwa mali zao.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, leo Mkurugenzi wa kampuni hiyo Dk. Scholastika Kevela, alisema amepewa maelekezo na serikali kupitia AGITF kuchukua hatua za kuuza mali za wadaiwa hao ambapo katika orodha hiyo kuna vigogo na wafanyabiashara wakubwa nchini.

Dk. Scholastika ameeleza, wadaiwa hao ni zaidi ya 200 ambao walikopa fedha na pembejeo mfuko huo wakiamini ni fedha za serikali zinatolewa bure hivyo kuto kurejesha.

“Serikali imeniagiza yoyote aliyechukua fedha katika Mfuko wa Pembejeo awe amerejesha ndani ya siku 14.Kama ulikopa uliwekeza nyumba tutauza fedha ya serikali irejeshwe,”amesema.

Amebainisha kiama hicho kitawakumba hata waliowadhamini wadaiwa hao kwani kwa mujibu wa sheria wanapaswa kulipa fedha hizo.

“Maana ya mfuko ni mtu kukopa kisha urejeshe ili mwingine akope lakini kuna baadhi walikopa katika mfuko huu na hawataki kurejesha. Wanaamini fedha hizi ni za serikali hivyo ni za bure tu. Tutawachukulia hatua,”amesema.

Dk. Scholastika amesema serikali ilianzisha mfuko huo kwa nia njema kwani vijana wengi hawana ajira hivyo wanauwezo wa kukopa fedha au pembejeo na kuanzisha miradi.

“Kwa niaba ya Mfuko wa Pembeje kama mdaiwa aliwekeza nyumba itauzwa ama kama aliwekeza gari kudhamini mkopo vitauzwa ili fedha ya serikali irejeshwe. Kukaa na fedha hii ni utovu wa fedha za umma,”amebainisha.

Aidha ameeleza operesheni ya kuzisaka na kuuza mali za wadaiwa hao itafanyika nchi nzima na katika orodha aliyokabidhiwa na serikali kuna vigogo, wafanyabiashara wakubwa na program kubwa za kilimo.

“Sheria inanibana kuwataja lakini wadaiwa wamo wafanyabiashara wakubwa waliochukua fedha hizi. Warejeshe haraka kwani serikali inazihitaji kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa shule, kugharimia elimu bila malipo, afya na barabara,”amesema.

Pia amewataka wananchi kutumia fedha za mikopo kwa malengo waliyo kusudia kuepuka kushindwa kurejesha fedha hizo ili zinufaishe watu wengine wanaohitaji kukopa kwa maendeleo.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...