Na Pamela Mollel,Babati

Wanafunzi 40 kutoka shule nne zilizopo ndani ya Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya Burunge (Burunge WMA) wilayani Babati, mkoa wa Manyara, wameanza ziara ya mafunzo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kujifunza masuala ya utalii na uhifadhi.

Wanafunzi hao, wakiongozana na baadhi ya wazazi wao, walimu, maafisa elimu, viongozi wa serikali za vijiji pamoja na viongozi wa Burunge WMA, wameanza ziara hiyo leo Desemba 15 na inatarajiwa kukamilika Desemba 18. Ziara hiyo imefadhiliwa na taasisi ya Chem Chem Association, mwekezaji wa shughuli za utalii wa picha na hoteli za kitalii katika eneo la Burunge.

Akizungumza wakati wa kuwaaga wanafunzi hao, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda, amesema wanafunzi hao wanatarajiwa kuwa mabalozi bora wa utalii na uhifadhi katika jamii zao, hususan ndani ya Burunge WMA.

Kaganda amesema Burunge WMA, lililopo kati ya Hifadhi za Taifa za Tarangire na Manyara, lina umuhimu mkubwa kwa taifa kutokana na kuwa ni eneo la mapito ya wanyamapori na kichocheo muhimu cha sekta ya utalii.

“Tunatarajia nyie mtakuwa mabalozi wa kulilinda eneo hili ili lisivamiwe wala kuharibiwa, bali lihifadhiwe kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” amesema Kaganda.

Ameongeza kuwa mwanzilishi wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alianzisha hifadhi za taifa kwa lengo la kuwanufaisha Watanzania, na urithi huo unapaswa kuendelezwa na kurithishwa kwa vizazi vijavyo.

Aidha, ameipongeza Chem Chem Association kwa kufadhili ziara hiyo ya mafunzo, akisisitiza kuwa itawasaidia wanafunzi kuona kwa vitendo manufaa ya uhifadhi na utalii.

Hata hivyo, Kaganda amesema jukumu la kuandaa mabalozi wa utalii na uhifadhi lilipaswa pia kufanywa na viongozi wa Burunge WMA, ambao hupata zaidi ya shilingi bilioni 1.7 kwa mwaka kutokana na mapato ya utalii.

“Ninaagiza watoto hawa wakirejea, uongozi wa Burunge WMA ukae nao na kuwaeleza kwa kina faida za uhifadhi, mapato wanayopata kila mwaka na mgao wa fedha unaorejeshwa kwa kila kijiji,” amesema.

Awali, Meneja Mkuu wa Chem Chem Association, Clever Zulu, amesema wanafunzi hao wamechaguliwa baada ya kufanya mitihani ya masuala ya uhifadhi na kufanya vizuri.

Zulu amesema mradi huo ulizinduliwa mwaka huu na unatarajiwa kuwa endelevu ili kila mwaka kuzalisha mabalozi wengi zaidi wa utalii na uhifadhi nchini.

“Tunaamini watoto hawa wakirejea watakuwa chachu ya kuhamasisha jamii zao kuthamini na kulinda rasilimali za utalii,” amesema Zulu.

Ameongeza kuwa Tanzania imebahatika kuwa na vivutio vingi vya utalii, ikiwemo wanyamapori, ambavyo vinahitaji kulindwa kwa wivu mkubwa ili kuendelea kuchangia uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Sangaiwe, kilichopo ndani ya Burunge WMA, Marian Mwanso, ameishukuru Chem Chem Association kwa kuwasaidia wanafunzi na wazazi kupata fursa ya kujifunza masuala ya utalii na uhifadhi.

“Mwekezaji huyu amekuwa na ushirikiano mzuri na vijiji vinavyozunguka Burunge WMA, na kijiji chetu cha Sangaiwe kimenufaika kwa kiasi kikubwa kupitia shughuli za utalii,” amesema Mwanso.




Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...